Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Waitara asisitiza mawasiliano TAZARA


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), sehemu ya Tanzania kuboresha mawasiliano kati yake na wafanyakazi ili kuleta ufanisi wa utendaji kazi wa Mamlaka hiyo.

Aidha, amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Uchukuzi kutuma wataalam wake katika Mamlaka hiyo na kusikiliza changamoto zao pamoja na ktafuta suluhu na kuziwasilisha kwa uongozi wa juu kwa hatua za uboreshaji.

Naibu Waziri Waitara ameyasema hayo jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili katika Mamlaka hiyo kuzungumza na uongozi na wafanyakazi na kukagua karakana inayokarabati mabehewa ya reli ya tazara.

“Nimebaini Mamlaka haina mawasiliano mazuri kati ya menejimenti na wafanyakazi, ndio maana kumekuwa na manung’uniko mengi kutoka kwa baadhi ya watumishi”, amesisitiza Naibu Waziri Waitara.

Ameeleza umuhimu wa mawasiliano na ushirikishwaji wa watumishi katika hatua zote zinazofanyika za utekelezaji wa miradi katika mashirika ya umma kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini kwa uwazi ili kuepusha sintofahamu na malalamiko ya ndani.

“Hata kama unafanyakazi nzuri kiasi gani wenzako wakilalamika ujue kuna sehemu mmeachia mianya ya watumishi kuwafikiria wanavyotaka hivyo kila jambo linalofanywa na uongozi lazima kuwepo na uwazi ndani yake”, amefafanua Naibu Waziri Waitara.

Naye, Meneja wa TAZARA sehemu ya Tanzania Bw. Fuad Abdallah, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa urefu wa reli ya TAZARA kuanzia Dar es Salaam hadi Kapiri Mposhi ni kilometa 1,860 na kati ya hizo kilometa 975 zikiwa Tanzania na 835 zikiwa zipo Zambia.

Ameongeza kuwa reli ya TAZARA ina unganisha Tanzania na nchi zote za SADC ikiwa na upana wa milimita 1,067 na kusafirisha watalii kutoka South Afrika kupitia Zambia hadi Tanzania.

Amueleza pia kiwango cha kusafirisha mizigo katika Mamlaka hiyo imepanda kutoka tani 87 za mwaka 2014 hadi tani 500,000 huku mizigo mingi inayosafrishwa inatoka katika nchi za Zambia na Kongo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi kanda ya Dar es Salaam, Bw. Jacob Shindika, ameiomba Serikali kuliangalia Mamlaka hiyo kwa jicho ka kipekee kuhusu malipo ya mishahara ya wafanyakazi ambapo kuna baadhi hadi sasa hawajalipwa stahiki zao.