Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA MSALATO WAFIKIA ASILIMIA 72.


Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imeridhishwa na Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato jijini Dodoma ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 72 kwenye Barabara ya kuruka na kutua ndege huku Jengo la abiria likifikia asilimia 39.

Hayo yamesemwa leo Agosti 30, 2024  na Msimamizi wa Mradi, Mahona Luhende wakati akitoa maelezo kwa kamati hiyo ilipotembelea mradi wa Ujenzi wa kiwanja hicho ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara ya kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Mpaka sasa utekelezaji wa miundombinu ya barabara umefikia asilimia 72 na kwa upande wa Majengo ni asilimia 39 na tunatarajia Novemba 2025 ujenzi wa miundombinu yote itakuwa imekamilika" amesema Mahona.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Yahya Rashid Abdullah ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea na Ujenzi wa miradi ya Kimkakati inayotoa taswira ya Nchi Kimataifa ambayo inatekelezwa kwa matumizi ya muda mrefu.

"Tumejifunza mengi kwa wenzetu kwani wao wanaangalia malengo ya muda mrefu na sio muda mfupi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara na viwanja vya Ndege"- amesema Yahya.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS)  mkoa wa Dodoma Mhandisi Zuhura Amani amesema mradi huo utakamilika Kwa wakati na changamoto zinazojitokeza zipo ndani ya uwezo na hazizuii utekelezaji na ukamilishaji na mradi huo.

"Tutakamilisha mradi kwa wakati na changamoto zilizopo haziwezi kutuzuia, tunawaahidibwananchi wa Dodoma na mikoa jirani watanufaika na mradi huu katika shughuli zao za kiuchumi"

Kamati hiyo imetembelea mradi wa Barabara ya Mzunguko wa Nje (Outer Ring Road) ya mkoa wa Dodoma yenye urefu wa kilometa 112.3 pamoja na Kiwanja cha Ndege Cha Kimataifa Msalato mkoani Dodoma.