Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

UTENDAJI BANDARI YA MTWARA WAONGEZEKA


Imeelezwa kuwa maboresho makubwa yaliyofanywa katika bandari ya Mtwara yameongeza tija na utendaji wa bandari kwani takwimu zinaonyesha kukua kwa tani zilizohudumiwa kutoka laki 5 mwaka 2021/22 hadi milioni moja kwa mwaka 2022/23 na meli zilizohudumiwa kutoka 166 kwa mwaka 2021/22 hadi 180 kwa mwaka 2022/23.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa kamati ya Maboresho ya huduma za bandari kwa bandari ya Mtwara mkoani Mtwara, Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi, ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu-Uchukuzi Mhandisi Aron Kisaka amesema Serikali imedhamiria kuongeza ufanisi wa bandari zote nchini kwa kushirikisha wadau katika hatua zote za uendeshaji ili kuhakikisha zinakuwa na ufanisi mkubwa.

“Serikali imedhamiria kuhakikisha pato linalokusanywa kupitia bandari linavuka asilimia 50 na utekelezaji wa hili ulianza kwa kufanya maboresho ya miundombinu na sasa inakwenda na mkakati wa kushirikisha wadau ili kuja na suluhu ya pamoja kwa changamoto zinazojitokeza amesema Mhandisi Kisaka.

Mhandisi Kisaka ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inaongeza juhudi kwenye masoko ili kuruhusu mashirika mengi zaidi kutumia bandari ya Mtwara hususani wakati huu ambao kuna mzigo mkubwa wa makaa ya mawe.

Aidha, Mhandisi Kisaka amesema Serikali inaendeleza juhudi za kuhakikisha inawakutanisha wadau wa ndani na wa nje hadi kufika mwezi Juni Wadau wa Tanzania na Zambia watakutana Tunduma lengo likiwa kujadili na kutafuta muarobaini wa changamoto za usafirishaji katika ukanda wa kusini mwa Tanzania.

Kwa upande wake Meneja wa bandari ya Mtwara Norbert Kalembwe, amesema kupungua kwa tozo kwa bidhaa mbalimbali zinazosafirishwa kupitia bandari hiyo kumechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa mizigo.

Meneja Kalembwe ametumia fursa hiyo kuwataka wadau kujipanga kwa ajili ya msimu wa korosho kwani amewahakikishia kuwa makontena yapo na maeneo ya kuhifadhia mzigo yameshatengwa.

Serikali kupitia TPA imekuwa ikikutana na wadau wa bandari mara moja kwa mwezi lengo likiwa kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati na kwa kushirikisha wadau wote ili kuongeza ufanisi wa bandari hizo.