Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

UPEMBUZI YAKINIFU BARABARA YA KARATU-MANGOLA-SIBITI WAKAMILIKA


Serikali imesema imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya njia panda (Karatu) – Mangola – Matala – Sibiti River hadi Lalago yenye urefu wa kilometa 328 inayojulikana kama “Eyasi Route”.

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, amesema hayo bungeni leo wakati akijibu swali la Mheshimiwa Daniel Tlemai Awack, Mbunge wa Karatu, aliyetaka kujua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.

Naibu Waziri Kasekenya ameliambia bunge kuwa Sehemu ya kuanzia Sibiti River hadi Lalago yenye urefu wa kilometa 121 imejumuishwa kwenye mradi wa EPC +F kupitia barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa (km 389) ambayo mkataba wake wa ujenzi umeshasainiwa.

Amesema sehemu iliyobaki ya Njia Panda ya (Karatu) – Mangola hadi Matala (km 137), Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Aidha, Eng. Kasekenya amesema kuwa Serikali bado inatambua umuhimu wa barabara ya Liwale hadi Mahenge kwa wananchi kwa kuwa  inapitika katika Hifadhi ya Mwalimu Nyerere.

“Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiulinzi na kijamii na barabara hii kuunganisha Mikoa ya Lindi na Morogoro, imetenga jumla ya Shilingi milioni 143.04 kwa ajili ya kazi za Upembuzi Yakinifu wa Awali”, amesema Eng. Kasekenya.

Ameongeza kuwa Kazi ya Upembuzi Yakinifu wa Awali itakapokamilika katika Barabara hiyo inayopita katika Hifadhi ya Mbuga ya Wanyama ya Selous itaonesha iwapo mradi unakidhi vigezo vya uhifadhi mazingira ili kuwezesha kujengwa.

Mheshimiwa Kasekenya alikuwa akijibu hayo katika mkutano wa 12 kikao cha Tisa cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililoahirishwa leo.