Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ULEGA AKAGUA VIFAA VYA KUKABILIANA ATHARI ZA EL NINO


 

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza kufanyika kwa ukaguzi wa barabara na madaraja yote nchini kama sehemu ya maandalizi dhidi ya mvua kubwa za El-Nino zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Ulega amesema ukaguzi huo ndiyo utakuwa msingi wa kufahamu ni wapi na wapi panahitaji kufanyiwa kazi ili mvua hizo zisiathiri mzunguko wa watu na biashara.

“Naagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha barabara na madaraja yote nchini yanakaguliwa na hatua za haraka kuchukuliwa ili miundombinu hiyo iendelea kutoa huduma hata wakati wa mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini”, alisema Ulega.

Ulega ametoa maelekezo hayo akiwa mkoani Pwani katika ziara yake aliyoianza ya ukaguzi wa maandalizi ya kimiundombinu kufuatia maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa watendaji wa Serikali kuhakikisha nchi inakingwa na athari mbaya za mvua hizo.

Katika ziara yake hiyo, pamoja na mambo mengine, Waziri Ulega alikagua pia vifaa mbalimbali vitakavyotumika kufanya matengenezo ya dharura katika miundombinu ya barabara na madaraja nchini kote.

“Niwatake wataalam wa TANROADS kuwa na utayari wa kufanya kazi katika tahadhari hii ya mvua za El-Nino na kuhakikisha madaraja na makalavati yanakaguliwa, yanasafishwa ili yawe huru kupitisha maji pamoja na kuhakikisha hakuna barabara ya kitaifa inayofungwa,” amesisitiza Ulega.

Ulega amesisitiza kuwa pamoja na uwepo wa vifaa na mitambo, utayari wa wataalam na watendaji ndio msingi wa kuhakikisha nchi inapita salama katika kipindi cha mvua hizo.

Aidha, Ulega ameagiza Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na TANROADS kufanya tathmini ya kila wiki katika mikoa yote nchini, ili kubaini maeneo yoyote yanayohitaji kuongezewa nguvu kwa wakati.

 

Ulega amebainisha kuwa katika kuhakikisha huduma za dharura zinafika kila kona ya nchi, TANROADS imejipanga katika kanda mbalimbali na Mkoa wa Pwani ndio kitovu cha kanda zote kwa ajili maandalizi ya tahadhari ya mvua za El-Nino.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani, Mhandisi Joel Mwambungu, ameeleza kuwa Wakala huo umejipanga kukabiliana na athari za mvua hizo kwa ununuzi na usambazaji wa vifaa vya dharura katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwambungu amesema TANROADS tayari ina kalavati za chuma zenye jumla ya mita 5,638 ambazo zitakazotumika katika maeneo ambayo barabara au madaraja yanaweza kupata athari kutokana na mvua kubwa.

Amesema pamoja na kalavati hizo, TANROADS imeandaa vifaa vingine vya dharura kwa ajili ya kuhudumia mikoa yote nchini vikiwemo madaraja ya chuma saba (Mabey Bridge), huku vikapu vya kubeba mawe, makalavati ya plastiki yenye jumla ya mita 1,200 pamoja na kalavati nyingine za chuma zikiwa sehemu ya vifaa vinavyotumika katika maandalizi hayo.