Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Ujenzi wa Meli ya Mv. Mwanza wafikia asilimia 54


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa meli mpya ya MV. MWANZA inayotekelezwa katika Bandari ya Mwanza Kusini ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 54.

Prof. Mbarawa amezungumza hayo jijini Mwanza, katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea na kuwataka wasimamizi wa mradi huo kuusimamia mradi huo ili ipatikane thamani ya fedha iliyotumika.

Prof. Mbarawa ameeleza kuwa ujenzi wa meli hiyo haujasimama kama taarifa zinazotolewa na watu wengine na kusisitiza kuwa msimamizi na mkandarasi wapo eneo la kazi usiku na mchana kuhakikisha meli hiyo inajengwa kwa viwango.

“Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi wa meli hii na Serikali inaendelea kutoa fedha za mradi kwa wakati, hivyo mradi haujasimama kama watu wengine wanavyozusha”, amesema Prof. Mbarawa.

Ameeleza meli hiyo inayojengwa kwa gharama zaidi ya shilingi Bilioni 89 itakuwa na madaraja matatu, maeneo ya watu mashughuli (VIP), vyumba vya mikutano, uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 na magari madogo 20.

Aidha, ameeleza changamoto iliyokabili mradi huo kuchelewa ni kutokana na kuanza ujenzi wa meli bila ya kuwa na chelezo ambapo hadi sasa ujenzi wa chelezo umekamilika na kazi zinaendelea.

“Hii meli imechelewa kwa sababu moja tu huwezi kujenga meli na chelezo pamoja kwanza unaanza chelezo halafu unakuja kujenga meli”, amefafanua Prof. Mbarawa.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Philemon Bagambilana, amesema kuwa ujenzi wa msingi wa meli hiyo kwa asilimia kubwa umekamilika na inatarajiwa kushushwa majini ifikapo mwezi Aprili au Juni huku ikiendelea kujengwa kwenye maji.

Naye, Meneja wa Mradi Luteni Kanali Mhandisi Vitus Mapunda, amemuhakikishia Waziri kuwa ujenzi wa meli hiyo unasimamiwa kwa karibu kwa viwango vinavyohitajika katika meli za aina hiyo.

Ujenzi wa Meli ya MV. Mwanza unatekelezwa na  Kampuni ya Gas Entec Company Limited ikishirikiana na kampuni ya Kangnam Corporation zote kutoka Korea Kusini zikishirikiana na SUMA JKT ya Tanzania ambapo mradi unatarajiwa kukamilia ifikapo mwezi Septemba, 2022.