Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Moshi waiva


Imeelezwa kuwa katika kuhakikisha huduma za utalii na usafiri wa anga zinaimarika katika mkoa wa Kilimanjaro Serikali itakifanyia ukarabati mkubwa kiwanja cha ndege cha Moshi.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Godfrey Kasekenya alipokagua kiwanja hicho na kusisitiza kuwa tayari kiasi cha shilingi bilion kumi zimetengwa kwaajili ya kukiboresha kiwanja hicho awamu ya kwanza.

Amewataka  wadau wa utalii mkoani Kilimanjaro kuweka mazingira bora ya kukuza utalii wa mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kwa kutumia kiwanja hicho kikamilifu.

Naibu Waziri huyo ameutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha mkandarasi wa kiwanja hicho anapatikana kwa haraka na kuitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), kuboresha huduma katika kiwanja hicho ili kuvutia wadau wengi kutumia.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro Eng. Motta Kyando amesema ukarabati wa kiwanja hicho utahusisha urefushaji wa njia ya kutua na kuruka ndege ambayo  itajengwa kufikia urefu wa mita 1,300 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa uzio na barabara za kuzunguka kiwanja hicho na barabara ya maingilio ya kwenda katika kiwanja hicho.

Amesisitiza kuwa maandalizi yote yako katika hatua za mwisho hivyo amewataka watakaopata fursa katika ukarabati huo kufanya kazi kwa uzalendo,

Naye Mbunge wa Moshi mjini Mhe. Priscus Tarimo ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kukikarabati kiwanja hicho na kusisitiza kuwa ukarabati huo utaboresha  biashara na utalii katika mkoa wa Kilimanjaro na kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kaimu Meneja wa kiwanja hicho Eng. Dickson Mmbando amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa kiwanja hicho kikikarabatiwa kitavutia wasafirishaji wengi wa anga kukitumia na kuongeza tija kwa wananchi.

Kiwanja cha ndege cha Moshi ni miongoni mwa viwanja 59 vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), na miongoni mwa viwanja vikongwe hapa nchini ambapo kilifunguliwa mwaka 1954 kikijulikana kama Moshi Aerodrome & King George VI Playing Field.