Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Tutaendelea kuimarisha miundombinu ya Uchukuzi Prof. Mbarawa


WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya uchukuzi kwa nyanja zote ili kukuza biashara na utalii hapa nchini.

Akipokea ndege mpya ya Edelweiss Airbus A 340 ikiwa na watalii 270 toka Zurich Uswis iliyoanza kutoa huduma zake kati ya Zurich Uswis na Kilimanjaro na Zanzibar hapa nchini, Prof. Mbarawa amesema hatua hiyo itaongeza fursa za ajira kwa kuwa itachochea shughuli za utalii na biashara nchini.

"Kuanza kwa safari za ndege hii kunaonesha kuwa Tanzania iko salama kwa wageni na wenyeji hivyo juhudi za mapambano dhidi ya Uviko 19, zitaendelea ili kuhuisha tena huduma za utalii na biashara," amesema Prof. Mbarawa.

Aidha ameushukuru uongozi wa Kampuni Edelweiss kwa kukubali kuanza safari kati ya Uswis na Tanzania na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa kwa kutoa huduma bora za biashara na utalii.

Amesisitiza kuwa kuanza kwa safari hizo kati ya Zurich Uswis, Kilimanjaro na Zanzibar ni mkakati wa Serikali kuimarisha huduma za utalii na biashara.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro amesema kupokea abiria 270 toka Uswis kuja kutalii nchini ni ishara njema kwa sekta ya utalii na kuwataka Watanzania kuendeleza hulka za ukarimu kwa wageni ili kuvutia wageni wengi zaidi na hivyo kukuza utalii na biashara kwa ujumla.

Kwa upande wake, Balozi wa Uswis nchini Tanzania, Didier Chassot amesema ubora wa utalii wa fukwe, mbuga na Mlima Kilimanjaro ndiyo umevutia watalii toka Uswis kuja moja kwa moja kutalii nchini.

Amesema kuanzia sasa ndege za Edelweiss Airbus zitafanya safari mara mbili kwa wiki toka Zurich Uswis hadi Kilimanjaro na Zanzibar.

Edelweiss inakuwa ndege ya pili toka kampuni ya Lufthansa kutoka Ulaya kuja moja kwa moja Tanzania kufuatia ndege yake nyingine ya Eurowings kuanza safari toka Frankfurt Ujerumani kwenda Zanzibar mara mbili kwa wiki tangu Julai mwaka huu.