Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TPA watakiwa kujipanga kufanya Biashara


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Bandari nchini kujipanga kufanya biashara ili kukidhi malengo ya Serikali ya kutumia lango la bandari kukuza uchumi wa nchi na wakazi wake.

Amesema Serikali inatumia fedha nyingi kujenga na kukarabati miundombinu ya bandari hivyo ni wakati sasa kwa watendaji na watumishi wa bandari kuleta biashara kubwa nchini itakayoleta faida na kuhuisha uchumi wa sekta nyingine.

“Ni wakati wa idara ya masoko ya bandari na watumishi wake kufanya kazi kimkakati wakilenga kufanya biashara na kuzalisha faida”, amesema Prof. Mbarawa.

Amezungumzia umuhimu wa watendaji wa bandari kuweka wahitimu wa fani za uhandisi katika miradi ya ujenzi inayoendelea ili kuwajengea watanznia uwezo.

Zaidi ya shilingi bilioni 440 zitatumika katika ukarabati mkubwa wa bandari ya Tanga na kukamilika huko kutawezesha meli nyingi na kubwa kutumia bandari hiyo na kufufua uchumi wa mkoa huo.

Amezungumzia umuhimu wa uadilifu, ubunifu na uzalendo kwa watumishi wa bandari ili waweze kushindana na bandari nyingine na kupata tija.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw, Adam Malima amemhakikishia Waziri wa Ujenzi  na Uchukuzi kuwa mkoa huo utahakikisha unaweka mazingira salama na rafiki kwa wakandarasi wanaojenga miundombinu mkoani humo ili kufikia malengo ya kimkakati ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Prof. Mbarawa alikuwa katika ziara ya siku tatu mkoani Tanga kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, vivuko, uwanja wa ndege na bandari.