Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TPA wapewa miezi Sita kukamilisha bandari kavu ya Kwala


WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ametoa miezi sita kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), kuhakikisha ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Ruvu mkoani Pwani unakamilika.

Akikagua maendeleo ya Ujenzi wa mradi huo ambao ulianza kujengwa tangu mwaka 2017, Profesa Mbarawa ameelezea kutokuridhishwa kwake na maendeleo ya mradi.

"...Sijaridhika na kasi ya ujenzi wa mradi huu hivyo nawataka TPA na SUMA JKT katika kipindi cha miezi sita ijayo kazi hii iwe imekamilika na nitakuwa nikija kila mwezi kukagua maendeleo ya mradi," alisema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa ameagiza mkataba wa ujenzi wa mradi huo urekebishwe, TPA wamlipe mkandarasi kwa wakati na kutafuta vifaa vinavyohitajika katika mradi kama saruji, kamera za usalama na kuhakikisha bei za vifaa zinaendana na soko.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Erick Hamis amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa mradi huo utakamilika katika kipindi cha miezi sita kama alivyoagiza ili kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuiwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

“Sisi TPA tunaihitaji sana Bandari hii kwani itatupunguzia msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kutoongezea nafasi ya kuhifadhi mizigo mingi zaidi, na hivyo kuongeza mapato.

Zaidi ya makontena 3,400 yanatarajiwa kuhifadhiwa katika Bandari Kavu ya Kwala itakapokamilika.

Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa Mradi huo, Kanali Samwel Machemba kutoka SUMA JKT ameahidi kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi, Prof. Mbarawa amepokea mabehewa 44 yatakayotumika katika Shirika la Reli nchini, TRC na kuwataka viongozi na madereva watakao yaendesha kuhakikisha yanatunzwa vizuri ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.

"...Tutaendelea kutoa fedha kwenye reli ya kati na SGR hivyo kazi yenu iwe kulinda miundombinu na kukusanya fedha," amesisitiza Profesa Mbarawa.

Aidha amezitaka taasisi zote zilizo chini ya wizara yake kufanya kazi kufikia malengo na zile zinazokusanya mapato msisitizo uwe kukusanya mapato.

Mapokezi ya mabehewa 44 ni sehemu ya mchakato wa uboreshaji wa reli ya kati, kati ya Dar es Salaam hadi Isaka, ambapo tayari ujenzi wa njia ya reli na madaraja umeimarishwa, ufufuaji wa vichwa vya treni na ukarabati wa mabahewa na injini za treni unaendelea.