Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TANZANIA YAAZIMISHA SIKU YA BAHARI DUNIANI


Imeelezwa kuwa usafiri wa baharini umekuwa na umuhimu mkubwa katika  usafirishaji wa mizigo duniani kwani takribani asilimia 80 ya biashara kimataifa hutegemea usafiri huo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya bahari duniani Wilayani Kilwa Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. Atupele Mwakibete, amesema kwa kutambua umuhimu huo Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa meli nane zikiwemo nne kwa Tanzania Bara na nne Zanzibar.

“Napenda kuwahakikishia kuwa Viongozi wetu wa Kitaifa wanatambua umuhimu mkubwa wa usafiri huu na uwekezaji huo ukikamilika utakuwa na manufaa kwa kuongeza pato la taifa kwa ujumla lakini pia kupunguza zaidi gharama za bidhaa zinazosafirishwa’, amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema pamoja na ujenzi wa meli hizo Serikali kwa Tanzania Bara inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu ya bandari za bahari ya Hindi na kwenye maziwa lengo likiwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria.

Naibu Waziri Mwakibete amelitaka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kuhakikisha linafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vya usafiri majini ili kuhakikisha vinakidhi matakwa ya uendeshaji kulingana na sheria za kimataifa za usafiri huo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Bi. Zainab Kawawa, ameipongeza Serikali kwa kuendeleza miundombinu na kusema kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa mkoani humo na itakuza utalii.

Mkuu huyo wa Wilaya ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendeleza bandari ya uvuvi ya Kilwa ambayo kukumilika kwa mradi huo kutasafirisha tani elfu 60 kwa mwaka.

Naye Muwakilishi wa Katibu Mkuu wa Uchukuzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira, Stella Katondo, amemhakikisha Naibu Waziri Mwakibete kuwa Wizara itaendelea kufuatilia kwa karibu shughuli za usafiri wa majini kwa kuzingatia miongozo ya Kimataifa.

Maadhimisho ya siku ya bahari Duniani yanafanyika kwa siku nne Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ambapo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Teknolojia mpya kwa  uchukuzi  baharini wa kulinda  mazingira.