Habari
ULEGA: VIJANA WASIFUKUZWE KAZI OVYO
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa maelekezo kwa Mameneja na wasimamizi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu nchini kuhakikisha wanalinda na kusimamia maslahi ya watanzania waliopata fursa ya kuajiriwa na Wakandarasi.
Agizo hilo limetolewa jijini Dar es Salaam wakati akikagua ujenzi wa miundombinu ya barabara Yaendayo Haraka Awamu ya Nne (BRT 4) sehemu ya Ubungo hadi Mwenge (km 13.5) na kupokea changamoto za vijana wa kitanzania kufukuzwa kazi wanapolalamika au kutotendewa haki ikiwemo kucheleweshewa stahiki zao na Mkandarasi China-Geo Engineering Corporation anayetekeleza mradi huo.
“Hii si kwa eneo hili tu bali ni kwa nchi nzima, Kijana anapokwenda kufanya kazi katika hii miradi isiwe tu mtu anaamka asubuhi anamfukuza kazi, Hapana badala yake waheshimiwe kwa ile kazi wanayoifanya na hata mikataba yao iwe ni mikataba yenye kutunza utu wao”, ameeleza Waziri Ulega.
Ulega amesisitiza kuwa kijana akifanya makosa au ukiukaji wa sheria, hatua zichukuliwe kwa mujibu wa kanuni za kazi, lakini si kuwafukuza tu kiholela na kuiagiza TANROADS kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha vijana wanafanya kazi katika mazingira salama na yenye haki.
“Nimeelekeza wataalam wetu walinde haki za vijana wa kitanzania na tutashindwa kuwatetea endapo vijana hao kama watakutwa na mambo ya ubadhilifu, udokozi na uvivu”, amebainisha Waziri Ulega.
Aidha, Waziri Ulega baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo kipande cha Ubungo - Mwenge, ametoa miezi miwili kwa Mkandarasi China-Geo Engineering kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kama mkataba unavyosema na sio vinginevyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega ametoa miezi miwili kwa Mkandarasi Shandong Luqiao Group anayejenga kipande cha Mwenge - Tegeta kuthibitisha uwezo wake wa kutekeleza mradi huo kwa kasi na ubora unaotakiwa na wakishidwa kutekeleza hilo Serikali itavunja mkataba na kutangaza zabuni upya ili kumpata Mkandarasi mwenye uwezo wa kukamilisha mradi huo.
Ulega amesema Mkandarasi huyo amekuwa akionesha uzembe na kutozingatia maelekezo ya Serikali licha ya kupewa muda wa kutosha kukamilisha mradi huo unaogusa maisha ya Watanzania moja kwa moja.
Ulega amesisitiza Serikali haitavumilia mkandarasi yeyote anayeshindwa kutekeleza kazi zake kwa uadilifu, nidhamu na kasi inayostahili, hasa kwa miradi yenye umuhimu kama barabara zinazoelekea maeneo ya makazi na biashara.
Ameongeza kuwa serikali ina dhamira ya kuhakikisha miradi yote ya miundombinu ya barabara inakamilika kwa wakati ili fedha za wananchi zitumike kwa tija na kuleta matokeo yanayoonekana.
