Habari
UJENZI MADARAJA BARABARA YA KUSINI WAFIKA PATAMU
📌Lengo Kusini kufikika muda wote
📌 Ulega asema kero za mvua kuwa historia
📌Ni baada ya Rais Samia kuchukua hatua
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amekagua na kuridhishwa na hatua mbalimbali za ujenzi wa madaraja ya dharura yaliyoko katika Mkoa wa Lindi ambayo utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 88.
Baadhi ya madaraja hayo ni yale yaliyojengwa katika maeneo ya Somanga, Njia Nne na Matandu ambako kuharibika kwa barabara katika maeneo hayo wakati wa majira ya mvua kulikuwa kunasababisha usafiri wa kwenda mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma mgumu.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Ulega aliwahakikishia Watanzania kuwa madaraja hayo yatakapokuwa yamekamilika kwa asilimia 100, mambo yaliyokuwa yakitokea miaka yote kipindi cha mvua za masika katika eneo la Somanga, Njia Nne na Matandu hayatarejea tena.
"Nimekagua na nimeridhishwa na maendeleo ya miradi hii, Kazi ni nzuri na kazi inatia moyo sana, naomba nitoe shukrani nyingi sana kwa Rais Dkt. Samia Suluhu ambaye aliidhinisha matumizi ya fedha ya zaidi ya shilingi bilioni 400 nchi nzima kwa ajili ya miradi ya dharura iliyotokana na mvua kubwa za El Nino na Kimbunga Hidaya. Hizi ni kazi za fedha hizo,” amesema Ulega.
Katika hatua nyingine, Ulega amewahakikisha Watanzania kuwa wakandarasi hawatalala bali watafanya kazi usiku na mchana ili hadi kufikia Disemba 24, 2025 madaraja hayo yawe yamekamilika.
"Hadi tarehe 24 Disemba tutakuwa tumekamilisha madaraja, barabara za maungio pamoja na kufunga taa za barabarani", amesisitiza Waziri Ulega.
Waziri Ulega amekagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Somanga Mtama (m 60) ambalo limefikia asilimia 89, Daraja la Kipatwa (m 40) limefikia asilimia 86.7, Daraja la Mikereng'ende (m 40) limefikia asilimia 90.06 na Daraja la Njenga (Matandu) lenye urefu wa mita 60 ambalo limefikia asilimia 86.67.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mohammed Nyundo, ametoa pongezi kwa Waziri Ulega pamoja na timu ya wataalamu kutoka wizarani na TANROADS kwa ujenzi wa madaraja hayo ambayo hivi sasa kazi kubwa zote zimekamilika. Pia alisema wameambiwa kuwa wananchi wataruhusiwa kupita kwenye madaraja hayo pale mvua zitakapokuwa zimeanza.
Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Emil Zengo, amefafanua kuwa katika Daraja la Somanga Mtama (m 60), mkandarasi amekamilisha ujenzi wa nguzo 43 zenye urefu wa mita 12, nguzo kuu tatu zinazobeba daraja, boriti za chuma na ameshamaliza kusuka nondo katika kitako cha daraja kwa ajili ya kumwaga zege.
