Habari
TANROADS YAPOKEA TUZO YA KIMATAIFA KUTOKANA NA MCHANGO WAKE WA KUBORESHA USALAMA WA BARABARA (SAFER ROAD)

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepokea tuzo ya heshima katika mashindano ya kimataifa ya usalama wa barabara, iRAP Gary Liddle Memorial Trophy, kutokana na mchango wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), katika kuboresha usalama wa barabara ili kupunguza hatari za ajali na kuhakikisha usalama wa watumiaji wote wa barabara, kupitia mpango wa Ten Step Plan Tanzania.
Tuzo hiyo imetolewa Jumatatu Februari 17, 2025, katika mkutano wa Ten Steps to 2030 for Safer Road Infrastructure Side Event uliofanyika katika jiji la Marrakech nchini Morocco, ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 4 wa Mawaziri kutoka Mataifa mbalimbali Duniani kuhusu Usalama Barabarani.
TANROADS ilikuwa ni miongoni mwa washindani watano walioteuliwa kutoka nchi 11, baada ya kushindanishwa na taasisi nyingine 12 duniani.
Mbali na TANROADS, taasisi nyingine zilizofikia hatua ya mwisho katika tuzo hii ni kutoka nchi za India, Australia, Peru, na Saudi Arabia.
Tuzo ya iRAP Gary Liddle Memorial Trophy hutolewa kwa mamlaka na Wakala za barabara duniani zinazofanya juhudi kubwa za kuondoa barabara zenye hatari kwa watumiaji wake.
Waziri Ulega ameipongeza TANROADS kupitia Mtendaji mkuu wake Eng. Mohamed Besta kwa kazi nzuri inayoliletea taifa heshima na kuitangaza nchi duniani.
Tuzo hiyo ambayo ni ya kudumu hutolewa kwa heshima ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya iRAP, tangu 20072022 Gary Liddle aliyefariki dunia mwaka 2023.