Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TANROADS KUKAMILISHA MZANI MPYA WA KISASA WA MIKUMI


Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TANROADS ipo mbioni kukamilisha ujenzi wa Mzani mpya wa kisasa wa Mikumi uliopo barabara kuu ya Morogoro - Iringa, pamoja na maboresho katika mizani ya mikese uelekeo wa barabara ya Dar-es Salaam - Morogoro kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9, hatua ambayo itakayosaidia kumaliza msongamano wa magari katika barabara hizo.

Mwakilishi wa Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro Mhandisi Mussa Kaswahili amesema hayo tarehe 18 Julai 2023, alipozungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya Meneja wa TANROADS wa mkoa huo Mhandisi Alinanuswe L. Kyamba mara baada kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mzani huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 80.

Amesema baada ya kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji na Usafirishaji katika barabara ya TANZAM Highway, Serikali iliona Mzani uliopo kwa sasa hautoshelezi mahitaji ya kupima magari kwa wingi, hivyo imeamua kufanya maboresho ya mzani uliopo pamoja na kujenga Mzani mwingine mpya na wa kisasa ili kuendana na mahitaji ya sasa.

Amesema maboresho yanayofanyika katika mizani hizo mbili ni pamoja na kuweka vifaa maalum [Sensor] ambavyo vitafanya kazi ya kuchuja na kutoa taarifa ya uzito wa gari husika, kama limezidisha mzigo ama la na kama halikuzidisha basi linaendelea na safari moja kwa moja bila kupita katika Mzani na lile lililozidisha mzigo litalazimika kupita kwenye mzani.

Mhandisi Kaswahili amemtaja Mkandarasi wa mradi huo ni Kampuni ya kizalendo CGI Construction Company Limited ya mjini Morogoro ambayo imepewa kazi hiyo mwezi Februari mwaka huu na inatarajiwa kukamilisha mradi tarehe 30 Septemba 2023.

"TANROADS inapenda kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hasaan kwa kuendelea kuwa karibu na Wananchi kwa kutenga fedha na kuzileta kwa ajili ya matengenezo kwenye maeneo yenye changamoto, lengo la upimaji wa magari ni kudhibiti uzito ili barabara zetu ziweze kudumu, natoa wito kwa Wananchi hasa wasafirishaji kutoa ushirikiano katika kutunza na kulinda barabara zetu" Amesisitiza Mhandisi Kaswahili.

Ameongeza kuwa TANROADS na Serikali haijivunii kuwa na tozo nyingi katika mizani "tunavyotoza kwa wanaozidisha mzigo tunataka kuondosha magari yenye uzito mkubwa ili kulinda barabara zetu ambazo tumejenga kwa gharama kubwa kwa fedha zetu wenyewe, tunataka watu watii na kufuata sheria".

Nao baadhi ya Madereva wanaotumia barabara hiyo Ismail Madunda na Vincent Mkimbila wamesema kukamilika kwa maboresho na ujenzi wa mzani mpya Mikumi kutasaidia kumaliza msongamano katika maeneo hayo na hivyo kuwafanya wasafiri na wasafirishaji kufika kwenye safari zao kwa wakati.

 

Akizungumza kwa niaba ya Wananchi wa eneo hilo Bwana Antony Michael amesema "Tunaushukuru uongozi wa Rais Samia kwa kutujengea mizani mpya na maboresho yanayofanyika hapa, mradi huu ukikamilika foleni hapa itakuwa byee byee na watu watafika kwenye shughuli zao mapema kabisa".