Habari
SHERIA YA MAJENGO MUAROBAINI WA GHARAMA ZA UJENZI NCHINI
Imeelezwa kuwa kukosekana na sheria moja inayosimamia shughuli za ujenzi wa majengo imekuwa chanzo cha kusababisha gharama kubwa za ujenzi nchini.
Mhandisi Ujenzi wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Geofrey Mwakasenga, amesema katika kukabiliana na hali hiyo tayari baraza hilo limekamilisha mchakato wa kuandaa andiko linaloainisha umuhimu wa Sekta ya Ujenzi na hivyo kuwezesha kutungwa kwa sheria itakayosimamia shughuli zote za ujenzi wa majengo nchini.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kuandaa mfumo bora wa kisheria, kanuni na miongozo itakayosimamia ujenzi wa majengo nchini na hivyo kuwezesha Sekta ya Ujenzi kuwa na sheria moja inayoongoza shughuli zote za majenzi na hivyo kuondokana na utaratibu wa kuwa na sheria nyingi zinazosimamia sekta hiyo na kuongeza gharama za ujenzi.
“Uwepo wa sheria ya majengo nchini utawezesha kuwepo kwa mfumo wa pamoja wa usimamizi wa ujenzi wa majengo wenye uwezo wa kudhibiti uharibifu wa mazingira, ubora, usalama na afya katika Sekta ya Ujenzi”, amesema Mhandisi Mwakasenga.
Amezitaja sheria zinazosimamia ujenzi wa majengo nchini kuwa ni sheria za mipango miji, sheria ya afya na usalama mahali pa kazi, sheria ya zimamoto na uokoaji, sheria ya mazingira, sheria ya ukandarasi na usajili pamoja na sheria zinazosimamia taaluma na wataalamu katika fani za uhandisi, ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi.
Changamoto zinazoikabili sekta ya majenzi kwa sasa ni kutosimamiwa vizuri kwa miongozo ya ujenzi, ubomoaji wa majengo kutosimamiwa ipasavyo na kutokua na viwango vya kitaifa vya majengo nchini.
Mhandisi mwakasenga amesema NCC inaendelea kutoa ushauri na msaada wa kitaalamu kwa wadau wa Sekta ya Ujenzi nchini kuhusu mambo yanayohusiana na sekta hiyo pamoja na kuhamasisha na kuweka mikakati ya kukuza, kuendeleza na kupanua sekta ya ujenzi nchini hususani kwa kujenga uwezo na ushindani wa wazawa ili waweze kushindana na kutekeleza miradi kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), ni chombo kinachohusika na uratibu wa Sekta ya Ujenzi nchini pamoja na uchagizaji wa maendeleo ya sekta hiyo kwa ujumla na lilianzishwa mwaka 1979 kwa sheria ya Bunge Na. 20 na lilianza kutekeleza majukumu yake rasmi mwaka 1981.