Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI YAWAKINGIA KIFUA WAKANDARASI WAZAWA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA BENKI YA DUNIA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameiomba Benki ya Dunia kupitia upya masharti ya manunuzi katika mikataba ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ili kutoa fursa kwa Wakandarasi wazawa kushiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Bashungwa ametoa ombi hilo katika kikao na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Nathan Belete na ujumbe alioambatana nao cha kujadili mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya Ujenzi, leo tarehe 21 Februari 2024 Dar es salaam.


Bashungwa ameeleza kuwa Masharti yanayowekwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayosimamiwa na kufadhiliwa na Benki ya Dunia yamekuwa yakiwabana Wakandarasi wazawa na kushindwa kushiriki kwa kutokidhi vigezo katika manunuzi.

 Pamoja na mambo mengine wamejadili na kupokea taarifa ya miradi inayoendelea kutekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia na maeneo ya kushirikiana kati ya Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Benki ya Dunia.
 

Aidha, Waziri Bashungwa ameushukuru Uongozi wa Benki ya Dunia kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika ufadhili wa miradi ya maendeleo, ujenzi wa barabara na miundombinu mingine nchini.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakurugenzi kutoka Wizara ya Ujenzi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) pamoja na Wataalamu.