Habari
SERIKALI YATOA BIL 24.4 UKARABATI MIUNDOMBINU YA BARABARA NA MADARAJA PWANI

Serikali imetoa shilingi Bilioni 24.4 kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa Barabara na madaraja mkoani Pwani katika maeno Sita yaliyoathirika na mvua za El- Nino zilizonyesha Aprili 2024.
Akizungumza wakati alipotembelea miradi hiyo, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage, amesema kuwa TANROADS kupitia Kitengo cha ndani cha Ushauri wa Kihandisi cha (TECU) Mkoa wa Pwani kilifanya tathmini ya kina na kubaini maeneo sita makubwa yaliyoathirika kwa kiwango kikubwa ili kuyaafanyia ukarabati.
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni Kisauke, Kimange, karibu na Ruvu darajani, Kimanzichana, daraja la Mbambe na daraja la Mkapa.
Amefafanua kuwa katika eneo la Kisauke, Serikali imejenga daraja jipya lenye urefu wa mita 20 na midomo minne, na mradi huo ulikamilika Septemba 1, 2025 ambapo awali maji ya mto Wami yalivunja kingo na barabara ya Makurunge – Saadani – Mbuyuni, hali iliyosababisha usumbufu kwa watalii.
Ameongza kuwa katika eneo la Kimange, TANROADS imejenga box culvert lenye urefu wa mita 10 na kukamilika Septemba 1, 2025 ambapo awali daraja dogo lililokuwepo lilishindwa kupitisha maji yote, jambo lililosababisha magari kusubiriana kwa muda mrefu.
Kadhalika, ameeleza kuwa eneo la Ruvu darajani ambalo limekuwa likikumbwa na mafuriko kila msimu wa mvua nalo limekamilika kwa ukarabati na linaendelea kutumika huku eneo la Kimanzichana ambalo tuta lake liliathirika vibaya, nalo limekamilika na linaendelea kutumika.
Kwa upande wa daraja la Msimbagenge lililokatika barabara ya Bungu – Nyamisati, Serikali ilijenga daraja jipya lenye urefu wa mita 10, midomo miwili na kina cha mita nne ambapo ujenzi wake ulikamilika Agosti 2025 na linaendelea kutumika.
Aidha, Meneja huyo wa TANROADS Mkoa wa Pwani amesema, eneo pekee ambalo bado linaendelea na ukarabati ni daraja la Mkapa katika eneo la Ikwiriri, ambapo makalvati yote yamekamilika na ujenzi wa njia za maingilio unaendelea huku mradi huo ukitarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 25, 2025.