Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI YASISTIZA USHIRIKIANO NA AFDB


Serikali imewahakikishia wadau wa maendeleo kuwa itaendeleza ushirikiano  uliopo baina yake na wadau hao ili kuhakikisha mchango wa fedha wanazotoa kufadhili miradi mbalimbali ya miundombinu zinatumika na miradi inakamilika kwa wakati.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, jijini Dodom wakati alipokagua maendeleo ya Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), Jonatahan Nzayikorera ,na kusema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu bora na inayoweza kutumika majira yote ya Mwaka.

“Serikali inafarijika sana kama wafadhili mnapokuja kuona utekelezaji wa miradi hii, kwani inatupa faraja kuwa hamtoi tu fedha lakini mnakuja kuona wenyewe kwa macho kile tunachokifanya kupitia fedha hizi’ amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa ametumia fursa hiyo kumtaka Mkandarasi Kampuni ya Sinohydro Limited kuhakikisha inaongeza vifaa ili kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), Jonatahan Nzayikorera, ameipongeza Serikali kwa kutekeleza mradi mkubwa wa kiwanja cha Ndege na miradi mingine na kumuahidi Waziri Prof. Mbarawa kuwa Benki itaendelea kufadhili miradi ili kuwapa watanzania Miundombinu bora.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatus Mativila amesema mradi wa uwanja wa ndege umegawanyika sehemu mbili, sehemu ya kwanza itahusisha ujenzi wa Barabara ya Kuruka na kutua ndege yenye urefu wa km 3.6 na sehemu ya pili itahusisha jengo la abiria lenye uwezo wa kuchukua abiria milioni mbili kwa mwaka.

Mradi wa Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Msalato ambao umefikia zaidi ya asilimia 10 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2024 na awamu zote zinatajwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 350.