Habari
SERIKALI YAJA NA MUAROBAINI WA ENEO LA MTANANA KUJAA MAJI
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi Aisha Amour kuwasimamia wataalamu kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika eneo Mtanana katika barabara kuu ya Morogoro – Dodoma uwe umekamilika na kupitika vipindi vyote vya mwaka.
Aidha, Bashungwa amesema kuwa tatizo la kukatika mawasiliano ya barabara kutokana na mvua za Elnino zinazoendelea kunyesha katika eneo la Mtanana jijini Dodoma litakuwa historia mara baada ya Serikali kupata suluhu katika eneo hilo.
Ameyasema hayo leo Tarehe 19 Januari 2024, jijini Dodoma mara baada ya kukagua eneo hilo ambapo mnamo tarehe 9 Januari, 2024 alimuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mohamed Besta kufanya tathmini ya eneo hilo ambalo lilijaa maji na kusababisha barabara hiyo kufungwa majira ya asubuhi.
"Wananchi Kama mlivyosikia tathmini ilivyowasilishwa mbele yenu, tumekuja na mkakati wa muda mfupi na muda mrefu, mwezi Desemba au Januari mwakani tutakuja hapa Mtanana kufuatilia tena suala hili", amesema Bashungwa.
Bashungwa ameongeza kuwa Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo inaendelea kufanya tathmini ambapo pamoja na muarobaini wa kuleta suluhu katika eneo hilo pia kuona namna ya kuvuna maji ya mvua yanayotuama hapo.
Ametoa wito kwa watanzania kuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuacha kukata miti ovyo na kulima kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kwani kufanya hivyo kunasababisha mafuriko na kuweza kufunga mawasiliano ya barabara na kupelekea kuharibika kwa mundombinu hiyo.
Kadhalika, Amemuelekeza Katibu Mkuu Amour kuhakikisha usanifu wa eneo hilo unakamilika mapema ifikapo mwezi wa pili kama walivyopanga ili kazi za ujenzi wa makalvati na madaraja katika eneo hilo kuanza mara moja.
Bashungwa amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kupeleka fedha za dharura Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja ili fedha hizo kuweza kutumika endapo mawasiliano katika miundombinu hiyo yanapoharibika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mipango ya Mindombinu kutoka TANROADS, Eng. Iftar Mlavi, amesema kuwa tangu tatizo la kujaa maji katika eneo hilo kutokea kaguzi mbalimbali zimefanyika ikiwemo kuwa na timu ya uangalizi inayohusisha TANRAODS pamoja na jeshi la Polisi na kukutana na Wizara ya Kilimo ili kutafuta uwezekana wa kuwa na bwawa kwa ajili ya kuzuia maji yanayotiririka pamoja na kujengwa kwa makalvati makubwa.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Simon Mayeka amesema kuwa Wananchi wa Mtanana wanataka kuona suluhisho la kudumu linapatikana katka eneo hilo kwani shughuli za kuchumi zimekuwa zikisimama kutokana na kero ya kujaa maji katika ene hilo.