Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI YAAZIMIA KUENDESHA SHIRIKA LA NDEGE KWA FAIDA


Serikali imesema kuongeza idadi ya ndege na  viwanja vya ndege nchini ni miongoni mwa hatua inazochukua ili kuifufua na kuifanya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), kujiendesha kwa faida, kufungua biashara za ndani na nje ya nchi pamoja na kuboresha mizania.

 

Hayo yamezungumzwa  jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Dkt. Ally Possi, wakati akizungumza na menejimenti ya ATCL, na kusisisitiza kwamba pamoja na maboresho yanayofanyika kwa sasa Shirika linakamilisha mpango biashara wa muda mrefu ili kuhakikisha ATCL inajiendesha kwa faida pamoja  na kulipa madeni yaliyopo.

 

“Serikali imeendelea kuwekeza kwenye Shirika hili na niwahakikishie maboresho ya viwanja vya ndege nchini yatachochea kwa kiasi kikubwa ongezeko la mapato na hatimaye madeni yanayoripotiwa yatalipwa", amesisitiza Dkt. Possi.

 

Aidha, Dkt Possi ameipongeza Menejimenti ya ATCL kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka kuhakikisha changamoto mbalimbali zinazokabili Shirika hilo ikiwemo mabadiliko ya ratiba yanaripotiwa mapema kwa abiria ili kuwafanya abiria kuendelea kuliamini na  kutumia Shirika hiyo.

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Eng. Ladislaus Matindi, amemuhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa Shirika linaendelea kuboresha utendaji na huduma ili likue na kuendelea kuaminika kwa utoaji huduma bora kwa zaidi ya vituo 15 vya ndani ya nchi na zaidi ya vituo sita vya nje ya nchi inavyovihudumia.

 

Eng. Matindi ameongeza kuwa kwa mwaka huu Shirika linakamilisha mazungumzo na mashirika makubwa ya ndege kama KLM na Emirates ili kuboresha huduma pale itakapoanza safari zake kwa vituo vya Uingereza na maeneo mengine kimataifa.

 

“Tayari tunashirikiano na mashirika makubwa ya ndege kama Air India ambao wanachukua abiria wetu tunaowapeleka Mumbai kuwapeleka kwenye maeneo mengine, lakini kwa sasa tunakamilisha mazungumzo na KLM na Emirate ili kuboresha huduma pale tutakapoanza safari za Uingereza na maeneo mengine", amefafanua Eng. Matindi.

 

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa sasa ina ndege 11 ambazo ni Boeing 787 ndege mbili, A220-330 ndege nne, Dash 8-Q400 ndege tano na tayari Serikali inaendelea na manunuzi ya ndege nyingine tano ambazo zinatajiwa kuanza kuwasili nchini mwaka 2023