Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Serikali kufunga Rada Saba za Hali ya Hewa nchini


Serikali imeingia mkataba kwa ajili ya ujenzi wa rada mbili za mwisho za Hali ya Hewa ili kufikisha mtandao wa rada saba  zinazotarajiwa kufungwa katika mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro kwa ajili ya kuboresha ukusanyaji na utoaji wa taarifa za hali ya hewa nchini.

Aidha, Serikali imekwishafunga rada tano za hali ya hewa ambapo kati ya hizo rada tatu zimeshafungwa katika mikoa ya Dar es Salaam (Bangulo), Mwanza (Kiseke) na Mtwara (Mikindani) na tayari zimeshaanza kufanya kazi na rada mbili zitakazofungwa katika mikoa ya Mbeya (Kawetire) na Kigoma (Nyamoli) ziko katika hatua za mwisho za utekelezaji.

Ameyasema hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara akiwa jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambapo pamoja na mambo mengine ameipongeza Mamlaka hiyo kwa ufanisi na utendaji kazi mzuri ndani na nje ya nchi.

“Niwapongeze uongozi na watumishi wa Mamlaka hii kwani utendaji wenu umekidhi mahitaji ya ndani na nje ya nchi na kutunikiwa vyeti vya ubora wa huduma”, amesema Naibu Waziri Waitara.

Naibu Waziri Waitara amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kutobweteka na mazuri yanayoendelea kutekelezwa na Mamlaka hiyo na badala yake kuendeleza kubaini na kufatilia mwenendo wa hali ya hewa, vimbunga baharini, hali mbaya ya hewa, upepo mkali kwa ajili ya sekta za usafiri wa anga, majini, ulinzi, kilimo, uvuvi, utunzaji wa misitu na utalii.

“Taarifa mnazozitoa zinaleta tija kwa sekta zote kwani nimejaribu kufatilia sana hata watu wa meli, anga, kilimo na ujenzi wa miundombinu inayoendelea wanapata taarifa zote na kwa usahihi”, amesisitiza Naibu Waziri Waitara.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo na kuisimamia taasisi hiyo kwa ustawi wa maendeleo ya nchi yetu hasa katika karne ya sasa ambayo masuala ya tabia nchi yamekuwa mtambuka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi, amesema kuwa taasisi hiyo imeanzishwa mwaka 2019 chini ya Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 ikiwa na majukumu ya kutoa, kuratibu na kudhibiti huduma za hali ya hewa nchini.

Ameongeza kuwa Mamlaka hiyo ina mitambo ya kisasa pamoja na wataalamu ambao wamesaidia kuboresha sana utabiri kwani kiwango cha utabiri usahihi wake umefikia zaidi ya asilimia 80 hapa nchini.

Naibu Waziri Waitara yuko jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuzungumza na uongozi na watumishi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake.