Habari
DKT. MWIGULU: SERIKALI KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA BARABARA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara nchini ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyamikoma, wilayani Busega, mkoani Simiyu, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua umuhimu wa miundombinu ya barabara katika kukuza uchumi, hivyo imeanza kufanya maboresho ya mifumo ya kifedha ya mifuko mbalimbali, ikiwemo Mfuko wa Barabara.
Amesema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinaingizwa moja kwa moja kwenye mfuko husika ili kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa rasilimali fedha na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
“Serikali inawahakikishia wananchi kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi itaongezeka na kwenda kwa haraka zaidi kutokana na mabadiliko tuliyoyafanya,” amesema Dkt. Nchemba.
Aidha, Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itajenga barabara ya Nyashimo–Dutwa yenye urefu wa kilometa 48, huku akimpongeza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Boniface Mkumbo, kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu mkoani humo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amesema Serikali inatambua umuhimu wa kiuchumi wa barabara ya Mwanza–Nyanguge na imeendelea kuchukua hatua za kuiboresha ili kuhakikisha inakuwa katika hali nzuri ya kupitika.
Amesema Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na TANROADS ilianza kufanya ukarabati mkubwa wa kipande cha kilometa 100 cha barabara hiyo kilichokuwa kimeharibika kwa kiwango kikubwa, huku sehemu ya barabara kutoka mpakani mwa Mwanza kuelekea Musoma ikiendelea kufanyiwa marekebisho.
Kuhusu barabara ya Nyashimo–Dutwa yenye urefu wa kilometa 48, Waziri Kadogosa amesema upembuzi yakinifu umekamilika na wataalamu wanaendelea na hatua ya usanifu, ambayo imefikia zaidi ya asilimia 60.
Naye, Mbunge wa Busega, Mhe. Simon Songe, ameiomba Serikali kujenga barabara ya Nyashimo–Dutwa kwa kiwango cha lami akieleza kuwa ujenzi wake utarahisisha usafiri na usafirishaji pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.
