Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI KUJENGA KWA LAMI BARABARA YA LIKUYUFUSI–MKENDA


Serikali imesema imeanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Likuyufusi–Mkenda kwa kiwango cha lami, huku kipande cha kwanza cha Likuyufusi–Mukuru chenye urefu wa kilomita 60 kikitarajiwa kuanza kujengwa baada ya kukamilika kwa taratibu za malipo ya awali kwa mkandarasi.

Hatua hiyo inafuatia kusainiwa kwa mkataba kati ya Serikali na mkandarasi, huku fedha za malipo ya awali (Advance Payment) zikitarajiwa kutolewa wakati wowote ili kuwezesha kuanza kwa kazi za ujenzi.

Kauli hiyo imetolewa leo, Novemba 5, 2026, na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, wakati akijibu swali la Mbunge wa Peramiho, Dkt. Lazaro Komba, aliyetaka kujua lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha Tanzania na nchi jirani.

Akifafanua hatua za utekelezaji wa mradi huo, Kasekenya amesema ujenzi utafanyika kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza itahusisha kipande cha Likuyufusi–Mukuru chenye urefu wa kilomita 60.

Amesema Serikali inaendelea na taratibu za kuhakikisha fedha za malipo ya awali zinapatikana, huku mahitaji ya fedha hizo yakiwa tayari yamewasilishwa Wizara ya Fedha.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya mapitio na usanifu wa kina wa barabara ya Peramiho–Makoseni hadi Kilagano yenye urefu wa kilomita 82.97.

Amesema barabara hiyo pia imepangwa kujengwa kwa kiwango cha lami, ambapo baada ya kukamilika kwa usanifu na kujulikana kwa gharama halisi za ujenzi, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Kuhusu wananchi watakaopisha maeneo yao kwa ajili ya miradi hiyo, Kasekenya amewahakikishia kuwa hakuna atakayeondolewa katika eneo lake kabla ya kulipwa fidia stahiki kwa mujibu wa taratibu.

Amesema Serikali itahakikisha maandalizi ya fedha za fidia yanaenda sambamba na maandalizi ya fedha za ujenzi ili kulinda haki za wananchi watakaoguswa na utekelezaji wa miradi hiyo.