Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI KUENDELEA KUWEKEZA TAZARA


Serikali imesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga zaidi ya bilioni 12 kwa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo ya ndani na nje ya nchi hususani inayopitia bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Mbeya mara baada ya kutembelea stesheni, karakana na mgodi wa uzalishaji kokoto wa Kongolo, Naibu Waziri Atupele Mwakibete amesema TAZARA imekuwa ikisafirisha mzigo wa Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hivyo ili kuongeza idadi ya mzigo Serikali imeendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuhakikisha mzigo unawafikia walaji kwa wakati kupitia miundombinu bora.

“Nchi Jirani zinazotuzunguka zinatumia sana reli hii, na wateja hawa ni muhimu sana kuendelea kuwashawishi kutumia reli hii kupitia miundombinu mizuri na tusisahau biashara ni ushindani hivyo lazima tuliweke hili la maboresho kama kipaumbele’ amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa amewataka TAZARA kuhakikisha wanafanya ukarabati wa mara kwa mara wa stesheni zao nchini ili kupunguza changamoto mbalimbali zilizopo kwa sasa ikiwemo upungufu wa viti vya kukalia kwa abiria wanaposubiri kuingia kwenye treni.

Aidha, Naibu Waziri Mwakibete amesema ili mgodi wa Kongolo kujiendesha kwa faida ni wakati muafaka kwa TAZARA kuwa na mpango Madhubuti wa biashara ili kutumia vifaa vinavyonunuliwa kwa tija.

Kwa upande Mbunge wa Kyela na Katibu wa Wabunge wa Mkoa wa Mbeya, Ally Jumbe ameipongeza TAZARA kwa kuendeleza juhudi za mara kwa mara za ukarabati kwenye njia na kuhakikisha kuwa treni zinakuwepo na kuondoka kwa wakati.

Naye Meneja wa TAZARA Mkoa wa Tanzania Fuad Abdalla amesema miongoni mwa mikakati ambayo imeendelea kuchukuliwa ili kuongeza ufanisi na kuongeza pato ni pamoja na Mamlaka kuingia makubalino maalum na makampuni binafsi ikiwemo kampuni ya Calabash ili kuhakikisha kuwa reli hiyo inatumika wakati wote.

Meneja Fuad ameongeza kuwa TAZARA pamoja na changamoto za uchache wa vichwa vya treni na behewa Mamlaka imeendelea kuhakikisha inatumia vizuri  miundombinu iliyopo kwa kutoa huduma za viwango kwa kusafirisha abiria na mizigo kwa wakati.

Naibu Waziri Wa Uchukuzi Atupele Mwakibete yuko Mkoani Mbeya kwa ziara ya siku tatu kukagua miradi na miudnombinu inayotekelezwa na kusimamiwa na Sekta hiyo.