Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA AQRB, SEKTA BINAFSI KULETA USHINDANI SEKTA YA UJENZI


Serikali imesema inaendelea kushirikiana na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Sekta binafsi pamoja na wadau wengine wa Ujenzi ili kuhakikisha Sekta ya Ujenzi inakuwa shindani, endelevu na yenye mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.

Ameeleza hayo Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi, Rogatus Mativila wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa AQRB, Oktoba 15, 2025 jijini Arusha.

Aidha, Mhandisi Mativila ameelekeza Bodi hiyo kushirikiana na Wizara ya Ujenzi pamoja  na Ofisi ya Rais- TAMISEMI kuhakikisha miradi yote ya Umma inasimamiwa na wataalam waliothibitishwa ili kulinda ubora na usalama wa majengo.

Pia, ameitaka AQRB kuhakikisha inaboresha mifumo ya usajili na ufuatiliaji wa wataalam hao ili kudhibiti matapeli na makampuni yasiyo na usajili wa halali.

Kadhalika, amewataka wataalam hao kutumia mbinu za kisasa za Teknojia katika kubuni, kusanifu na kujenga ili kupata majengo bora, imara na ya kisasa ambayo yanaendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia.

Kwa upande wake, Kaimu Masajili wa AQRB Mbunifu Majengo, Daniel Matondo ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya Ujenzi na kuendelea kulinda taaluma hizo kwa sheria ambazo zimekuwa zikitungwa.