Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

RC Rukwa aipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu ya barabara


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Joseph Mkirikiti ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara nchini.

Ameyasema hayo wakati akifungua semina ya mafunzo kwa wadau wa usafirishaji kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inayofanyika kwa siku moja mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa, miundombinu ya barabara mkoani Rukwa imepitia changamoto mbali mbali, awali kutoka Tunduma hadi Sumbawanga ilikuwa ikichukua masaa nane hadi siku nzima hali kadhalika kutoka Sumbawanga kuelekea mikoa ya Tabora na Mwanza wananchi walikuwa wakipata mateso makubwa sana na ndio maana Serikali kupitia awamu tofauti imekuwa ikiweka msisitizo wa maboresho ya miundombinu kwa barabara zote nchini.

“Mkoa wa Rukwa unafunguka pande zote iwe kutoka Sumbawanga kwenda Tunduma, lakini pia kutoka Sumbawanga kwenda Tabora na Kigoma, hivyo tunalolijadili hapa ni suala pia la maendeleo ya mkoa wetu, iwapo miundombinu hii itatumika vizuri maana yake mkoa huu unaweza kuwa ni pito la bidhaa zinazotoka Congo DRC, hivyo kujipanga kimkakati katika utunzaji wa miundombinu ya barabara kunalenga kupandisha pato la mkoa wetu, lakini pia pato la Taifa.

“Mambo yote tunayo yajadili hapa yanahusu matumizi ya rasilimali za nchi hasa fedha kwa ajili ya maendeleo yetu, hivyo tunapojadili utekelezaji wa sheria hii ni lazima tutilie maanani dhana nzima ya uzalendo, kwani sheria inaweza kuwepo lakini kama hatutakuwa wazalendo katika kusimamia utekelezaji wake basi hatutakuwa tumefanya jambo jema”, amesema Mkirikiti.

Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi, Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa, Denis Bandisa, amewapongeza waandaaji wa mafunzo hayo kwa kuuchagua mkoa wa Rukwa kuwa mwenyeji wa semina ya mafunzo kwa wadau wa usafirishaji kuhusu Sheria ya Udhibiti uzito wa Magari na kuongeza kuwa jukwa hilo ni fursa moja wapo kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kukutana na wadau wa mkoa huo na kubadilishana mawazo.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Rukwa Mhandisi Mgeni Mwanga, amesema kuwa mafunzo hayo ni muendelezo wa utoaji elimu ya Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 ambayo yamekuwa yakitolewa kwa wadau wa usafiri wa barabara nchini tangu mwaka 2018 kabla ya kuanza kutumika rasmi kwa sheria hiyo mwezi Machi mwaka 2019.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau wa usafirishaji mkoani Rukwa, wameipongeza Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo kutokana na ukweli kwamba wengi wao hawana uelewa wa kutosha juu ya sheria hiyo ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki, na hivyo wamekuwa wakifanya makosa mengi kwa kukosa uelewa.

Semina ya mafunzo kwa wadau wa usafirishaji kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inayofanyika mkoani Rukwa imeandaliwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), na inahusisha wadau kutoka mikoa ya Rukwa na Katavi.