Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

PROFESA MBARAWA AZITAKA MENEJIMENTI ZA SEKTA YA UJENZI KUBUNI MBINU BORA ZA KIUTENDAJI


Menejimenti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) pamoja na taasisi zake wametakiwa kubuni mbinu za kiutendaji zinazolenga kuweka mazingira wezeshi yenye kuchochea na kuimarisha ari na morali kwa watumishi wanaowasimamia.

Wito huo umetolewa mkoani Tanga na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, wakati akifungua kikao kazi kati ya menejimenti ya Sekta hiyo pamoja na menejimenti za Taasisi zake ambazo ni TANROADS, TBA, TEMESA, RFB, ERB, CRB, AQRB, NCC, ICoT na Vikosi vya Ujenzi.

Amesisitiza kwa viongozi na watendaji hao kuwa huru kuelezana ukweli kuhusu masuala yanayohusu utendaji wa kisekta na kuleta mabadiliko ambayo yataongeza tija na uzalishaji katika Sekta hiyo.

"Kikao hiki madhumuni yake ni kuandaa mikakati na kupanga namna ya kuongeza ari na morali kwa watumishi kwa kuelezana ukweli na kutafuta majibu ya changamoto za watumishi kila kiongozi katika maeneo yao ya kazi" amesisitiza Prof. Mbarawa.

Amesema kuwa suala la morali kwa watumishi ni muhimu sana likapewa kipaumbele kwasababu morali ni kichocheo muhimu katika utendaji kazi.

"Morali ya watumishi ikiwa juu hapana shaka watajituma bila kusukumwa na kusaidia menejimenti zenu kuwasimamia kwa unafuu mkubwa", ameeleza Prof. Mbarawa.

Akitaja mafanikio yaliyofikiwa na Sekta hiyo, Prof. Mbarawa ameeleza kuwa TANROADS imekwisha tekeleza ujenzi wa barabara zenye urefu wa km 1,151.37 kwa kiwango cha lami na barabara zenye urefu wa km 4, 140.76 zimefanyiwa upembuzi yakinifu.

Miradi mingine ni ujenzi wa madaraja makubwa nane na madaraja mengine 6 tayari yameshafanyiwa upembuzi yakinifu na pamoja na uboreshaji wa viwanja vya ndege 19 ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake.

Mafanikio mengine ni upande wa TBA ambapo imetekeleza ujenzi wa nyumba za watumishi 150 kwa awamu ya kwanza, ujenzi wa nyumba 20 za viongozi zikiwa katika hatua mbalimbali na ujenzi wa nyumba za majaji katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Mafanikio mengine ni ujenzi wa vihenge vya kisasa na maghala ya kuhifadhia chakula katika mikoa nane nchini, usimamizi wa ujenzi wa majengo 17 na jengo moja la Ofisi ta Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama mkandarasi.

Mafanikio mengine kupitia TEMESA ikiwemo ujenzi wa vivuko vipya, ukarabati wa vivuko, ujenzi wa maegesho na miundombinu ya vivuko, ujenzi wa karakana mpya na vilevile mikataba ya ununuzi na usimikaji wa mifumo ya kieletroniki ambayo yote haya yatasaidia kutatua changamoto za miundombinu ya usafiri na usafirishaji.

Awali kabla hajamkaribisha Waziri Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Balozi Mha. Aisha Amour, ameeleza kuwa katika kikao hicho wataweza kubadilishana maarifa na uzoefu miongoni mwa watendaji wakuu wa Wizara na Taasisi zake.

"Kikao hichi kitajadili changamoto zilizopo za kitaalam na kitaasisi katika kutekeleza sera, mipango, program za Sekta ya Ujenzi na kupata mwelekeo sahihi wa utekelezaji wake", amesema Balozi Aisha.

Ameongeza pia kikao hicho kitajadili kwa mapana namna ya kusimamia na utekelezaji wa miradi tunapoelekea kuanza mwaka mpya wa fedha 2023/24.

Jumla ya watendaji 140 wameshiriki kikao kazi hicho kilichosheheni mada mbalimbali zikiwemo maarifa kuhusu uongozi na usimamizi, itifaki katika utumishi wa umma,utoaji wa maamuzi yanayojali hisia, utu na uondoaji wa msongo wa mawazo, miiko na utunzaji siri za Serikali katika utumishi wa umma.