Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Prof. Mbarawa: Ujenzi wa Reli ya Kisasa Isaka - Mwanza unaendelea


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kipande cha Isaka - Mwanza chenye urefu wa kilometa 341 unaendelea kwa kasi na mkandarasi yupo eneo la mradi na kazi zinaendelea. 

Prof. Mbarawa ameongeza kuwa Serikali imekwishalipa malipo ya awali kiasi cha shilingi Bilioni 376.36 kwa mkandarasi kwa ajili ya kuanza kazi za awali ikiwemo ujenzi wa tuta la reli na hadi kufikia hatua hiyo mradi unaendelea vizuri na Serikali haidaiwi. 

Ameyazungumza hayo jijini Mwanza, wakati akikagua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa kwa muda wa miezi 36 kwa gharama ya Sh Trilioni 3.062 unaojengwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction (CCEC), na China Railway Construction Corporation (CRCC). 

"Kazi zinaendelea mkandarasi amejipanga vizuri na tunategemea atakamilisha ujenzi huu kwa wakati kama ulivyopanga", amesisitiza Prof. Mbarawa. 

Aidha, Prof. Mbarawa ametoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za mradi huo kwa wakati kwa ajili ya manufaa ya wananchi na kusaidia kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika Ukanda huo. 

Awali akitoa taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa, ameeleza kuwa mradi huo ulianza mwezi Mei, 2021 na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2024. 

Amefafanua kuwa mradi huo unahusisha madaraja makubwa 43, vivuko vya chini 44, vya juu 23 na makalvati 591 na daraja refu eneo la kuingia Mwanza, vituo 9, stesheni kubwa ya Mwanza na pia kutakuwa na karakana kubwa eneo la Fela na Tabora kwa ajili ya reli hiyo. 

Bw. Kadogosa ameeleza pia tayari wamekwishalipa kiasi cha shilingi Bilioni 2.8 kwa ajili ya fidia za wananchi waliopisha mradi huo.