Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ONESHENI UWEZO TUWAPE MIRADI MINGI YA UJENZI ENG. KASEKENYA


Imeelezwa kuwa juhudi za Serikali za kuwawezesha kiutaalam, kiuzoefu na kimitaji kwa kuwapa miradi mingi ya ujenzi wakandarasi wa ndani ya nchi zitafanikiwa endapo wakandarasi hao watatambua dhima yao kwa nchi na kufanyakazi kwa bidii na viwango vya juu.

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya ameeleza hayo alipokagua ujenzi wa barabara ya Musoma – Makojo - Busekela yenye urefu wa KM 92 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umeanza sehemu ya Nyambui- Suguti.

“Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha wakandarasi wa ndani wanakuwa na uwezo na hivyo kujenga miradi mingi na mikubwa ili kukuza uchumi wa nchi na kuongeza fursa za ajira hivyo jitahidini kuongeza bidii na ubunifu”, amesema Eng. Kasekenya.

Amemtaka mkandarasi Gemen Engineering Co. Ltd, anayejenga barabara hiyo Km 5 za awali kutoka Nyambui - Suguti, kuhakikisha barabara hiyo inakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.

Akizungumzia umuhimu wa barabara hiyo Mkuu wa wilaya ya Musoma Dakta, Khalfan Haule amesema barabara hiyo inayopita eneo la Musoma vijijini ikikamilika litachochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa mkoa wa Mara kwa kuwa itaongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na shughuli za uvuvi.

Amesisitiza kuwa itachochea utalii kwa kuwa inapita pembezoni mwa ziwa Victoria hivyo kuongeza vivutio vya utalii mkoani Mara.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amemtaka Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Eng. Rogatus Mativila kufanya tathmini na kuja na majibu ya haraka ya namana bora itakayowezesha kasi katika ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Musoma.

Ameelezea kutoridhishwa kwake na kasi ndogo katika ujenzi wa uwanja huo na kusisitiza Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa wote wanaochelewesha miradi ya ujenzi kukamilika kwa wakati.

Naibu Waziri Kasekenya  yuko katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo pamoja na mambo mengine anahamasisha uwekezaji kwa wananchi pale inapopita miundombinu ya kisasa ili kujenga uchumi.