Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

NAIBU WAZIRI MWAKIBETE ATOA MWEZI UKAGUZI MT. SANGARA.


Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete ametoa mwezi mmoja kwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kutumia wataalam alionao kufanya tathmini ya kina kwa vifaa vyote vilivyofungwa kwenye Meli ya MT. Sangara na kuchukua hatua kwa taarifa itakayowasilishwa.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati huo mjini Kigoma na kubaini uwepo wa changamoto ya baadhi ya vifaa kuwa Naibu Waziri Mwakibete amesema Serikali haitaipokea meli hiyo itakapokabidhiwa na kugundulika kuwa na mapungufu.

“Nawakikishia vifaa vyote vilivyofungwa humu endapo itabainika baadae kuwa ni chakavu au vimeshatumika, Serikali itachukua hatua stahiki kwa wote waliohusika sababu changamoto zote za vifaa zinatakiwa kurekebishwa  sasa hivi” amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesisitiza umuhimu wa watalam kukagua kwa karibu ukarabati huo mkubwa unaofanyika  ili kuhakikisha maboresho yote yanayofanyika yanafanywa kwa kufuata vipengele vya mkataba.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Ester Mahawe ameishukuru Serikali kwa kufanya ukarabati wa meli hiyo na kusema kukamilika kwake kutarahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa mikoa inayozungukwa na Ziwa Tanganyika na nchi Jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa MSCL Philip Bangabilana amesema MSCL itaendelea kumsimamia kwa karibu Mkandarasi na kuhakikisha mapungufu yote yanarekebishwa kwa wakati kulingana na mkataba unavyoeleza.

Bangabilana ameongeza kuwa kwa sasa mradi wa Ukarabati wa MT. Sangara umefikia asilimia 66 na unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Novemba mwaka huu na kwa mwaka 2022/23 Serikali imetengea fedha kwa ajili ya meli nyingine mpya mbili.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mwakibete yuko mkoani Kigoma kwa ziara ya siku tatu kukagua miundombinu na miradi inayosimamiwa na Sekta ya Uchukuzi.