Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MSCL YATAKIWA KUTUMIA MELI KWA TIJA


Serikali imeitaka Kampuni ya  Huduma za Meli (MSCL) kuhakikisha inazitumia kwa tija meli tatu ilizokabidhiwa ili ziweze kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo kwa wakazi wanaozunguka Ziwa Nyasa na Nchi Jirani.

Meli hizo ambazo zimegharimu zaidi ya shilingi bilioni 10 ni MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 na mzigo wa tani 200, Mv. Ruvuma yenye uwezo wa kubeba mzigo wa tani 1000 na MV.Njombe yenye uwezo wa kubeba mzigo wa tani 1000.

Akizungumza Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya wakati wa makabidhiano hayo Mwakilishi wa Katibu Mkuu (Uchukuzi) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira -Uchukuzi Bi. Stella Katondo amesema kukabidhiwa kwa meli hizo katika kampuni hiyo inamaanisha kuwa  Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ambaye ndio mmiliki kubaki na kazi ya usimamizi wa bandari tu.

“Jukumu la TPA ni kusimamia bandari nchini si kuendesha meli ndio maana baada ya kukamilika kwa ujenzi wa meli hizi, Serikali ikaamua kuwakabidhi MSCL ambao ndio wenye dhamana ya kuendesha meli hizi, ni matumani yangu kuwa meli hizi zitatumika ipasavyo na tutaona thamani ya uwezekezaji huu”, amesisitiza Mkurugenzi Katondo.

Mkurugenzi Katondo amezitaka TPA na MSCL kuchukua jitihada za haraka za kutafuta na kushawishi wafanyabiashara wa makaa ya mawe na simenti ili kutumia meli hizo ili kusafirisha mzigo mkubwa zaidi, kwa gharama zinazohimilika na hatimaye kuwafikia walaji kwa wakati.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kyela Mhe. Ally Mlaghila amesema kukabidhiwa kwa meli hizo kwa MSCL kutaongeza tija kwa uendeshaji kwani kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa wa uendeshaji wa meli katika Ziwa Nyasa.

Naye  Mkurugenzi Mkuu wa Usimamizi wa  Bandari Tanzania (TPA)  Plasduce Mbossa  amesema tayari TPA imeshaanza mazungumzo na wafanyabiashara wa ndani na nchi zinazotumia ziwa Nyasa ili kuhakikisha mzigo unapatikana na zinatumika.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu MSCL Kapteni Samson Ng’wita, ameishukuru Serikali kwa kufanya maamuzi hayo na kusema kwamba MSCL iko tayari kuanza kuendesha meli hizo na kuahidi huduma bora na za viwango kwa abiria na wafanyabiashara.

Makabidhiano  hayo ya meli hizo tatu yamefanyika katika bandari ya Kiwira na kushuhudiwa na Uongozi wa Mkoa wa Mbeya, Wilaya ya Kyela, Mbunge wa Kyela, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango-Hazina, Katibu wa Chama Cha Mpainduzi -Kyela.