Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Mkuu wa wilaya ya Mtwara aipongeza Serikali kwa kuandaa mafunzo kwa wasafirishaji


Mkuu wa wilaya ya Mtwara Dustan Kobya, ameipongeza Serikali kwa kuandaa mafunzo kwa wasafirishaji kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018.

Ametoa pongezi hizo wakati akifungua semina ya mafunzo ya sheria hiyo kwa wadau wa usafirishaji yaliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), yanayofanyika kwa siku moja mkoani Mtwara katika ukumbi wa Chuo cha VETA.

“Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya yataongeza uelewa kwa Sheria hii ya Udhibiti Uzito wa Magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 kwa wasafirishaji hali itakayopelekea barabara zetu kudumu na kupitika nyakati zote na hivyo kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa gharama za matengenezo ya barabara mara kwa mara”, amesema Dustan Kobya.

Aidha Mkuu wa Wilaya huyo aliitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia TANROADS, kuandaa vipindi maalumu, majarida na vipeperushi vitakavyotoa uelewa zaidi kwa wadau wa usafirishaji, ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto ya uzidishaji uzito wa magari barabarani.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Meneja wa TANROADS mkoa wa Mtwara, Mhandisi Dotto John amesema kuwa, mafunzo hayo yanalenga kutoa uelewa kwa wasafirishaji ili kupunguza changamoto mbalimbali zitokanazo na uelewa mdogo wa Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari inayotumiwa na nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.

Kwa upande wake msimamizi wa Mizani kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Leonard Saukwa amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wasafirishaji na wamiliki wa magari ya mizigo ili waweze kuelewa sheria ya udhibiti uzito ya Afrika Mashariki na kanuni zake na kwamba watazunguka nchi nzima katika vituo 13 kwa ajili ya kutoa elimu hiyo

Mafunzo hayo ambayo yanashirikisha wadau mbalimbali wa usafirishaji yamepangwa kufanyika katika Mikoa 13 ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Morogoro, Dodoma, Njombe, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Geita, Tabora, Mwanza, Arusha na Tanga.