Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma awataka TANROADS kuongeza wigo wa utoaji elimu


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka ameutaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuongeza wigo wa utoaji elimu juu ya Sheria ya Afrika Mashariki ya udhibiti uzito wa magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018.

Ameyasema hayo wakati akifungua semina ya mafunzo ya sheria hiyo kwa wadau wa usafirishaji yaliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), yanayofanyika kwa siku moja mkoani Dodoma katika ukumbi wa Hazina

“Toeni elimu ya kutosha kwa wadau wa usafirishaji nchini, tumieni vyombo vya habari kwa kuandaa vipindi maalum vya redio na televisheni ili kuweza kuwafikia wadau wengi zaidi na hivyo kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa barabara hizi zinalindwa ipasavyo”, amesema Mtaka.

Ameongeza kuwa changamoto zinazowakumba watendaji wa mizani kutoka kwa wadau wa usafirishaji, zinatokana na baadhi ya wadau hao kukosa uelewa wa kutosha juu ya sheria ya Afrika Mashariki ya udhibiti wa uzito wa magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, amesema kuwa mafunzo hayo ni muendelezo wa elimu inayotolewa kwa wadau wa usafirishaji kuhusu sheria hiyo iliyoanza kutumika nchini Machi mosi mwaka 2019.

Mhandisi Chimagu amesema kuwa awali Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), ilifanya mafunzo hayo nchi nzima mwezi Oktoba mwaka 2020 na kwamba mafunzo hayo ni jukwaa muhimu la wadau wa sekta ya usafirishaji, kufanya majadiliano kuhusu sheria hiyo, kushauri au kutoa maoni yatakayostawisha utekelezwaji wake.

Aidha mmoja kati ya wadau wa usafirishaji Juma Mussa, anayeshiriki mafunzo hayo amewaambia waandishi wa habari kuwa uelewa juu ya sheria hiyo utawasaidia kudhibiti uzito wa magari yao na hivyo kuepukana na makosa wanayoyafanya kwa kukosa uelewa, hali itakayopelekea mtandao wa barabara nchini kudumu kwa muda mrefu bila kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.

Mafunzo ya Sheria ya Afrika Mashariki ya Udhibiti Uzito wa Magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 yamepangwa kufanyika katika Mikoa 13 ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Morogoro, Dodoma, Njombe, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Geita, Tabora, Mwanza, Arusha na Tanga, ambapo hadi kufikia sasa tayari, wadau wa usafirishaji katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Morogoro tayari wamenufaika na mafunzo hayo.