Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MIKATABA 15 YA UJENZI WA BARABARA YA ZAIDI YA TRILIONI 1 KUSAINIWA.


Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inatarajia kusaini mikataba 15 kwa pamoja ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami pamoja na Daraja zenye thamani ya shilingi Trilioni 1.034 ili kuboresha huduma za miundombinu nchini.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati akitoa majibu ya nyongeza leo Tarehe 03 Novemba, 2023 Bungeni jijini Dodoma katika kikao cha Nne, Mkutano wa 13.

Bashungwa amesema kuwa miradi hiyo inatarajiwa kutekelezwa kwa kutumia fedha za ndani za miradi ya maendeleo na Serikali iko mbioni kuandaa tukio hilo.

“Mheshimiwa Rais ameshatoa kibali kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivosema, na tumeona tuandae siku ambayo tutasaini mikataba hii kwa siku moja halafu baada ya hapo mimi na Naibu Waziri tutaambatana na Waheshimiwa Wabunge kwenda kuwakabidhi makandarasi kwenye majimbo yenu”, amesema Bashungwa. 

Awali Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa Busokelo, Mheshimiwa Atupele Mwakibete, amesema taratibu za manunuzi ya Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya barabara ya Katumba – Lupaso (km 35.3) na Kibanja – Tukuyu (km 20.7) zimekamilika, hatua inayofuata ni kumkabidhi mkandarasi eneo la kazi (signing).

Mheshimiwa Kasekenya alikuwa akijibu swali la Mheshimiwa Atupele Mwakibete Mbunge wa Busokelo aliyetaka kujua ni lini lini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Katumba – Mbambo hadi Tukuyu utasainiwa kwa kuwa Mkandarasi alishapatikana.