Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MELI ZA TPA MWAROBAINI WA USAFIRISHAJI WA ABIRIA NA MIZIGO ZIWA NYASA


Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ukarabati na kuanza kufanya kazi kwa meli ya MV. Mbeya II kutarahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa wasafirishaji walioko katika Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe na Nchi Jirani ya Malawi.

Akizungumza Wilayani Kyela Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema wananchi wa Mikoa hiyo wamekuwa wakilazimika kutumia mabasi bila na kuwa na njia mbadala ya usafiri hususani kwa wale wanaoishi mikoa hiyo hivyo kukamilika na kuanza kazi kwa meli hiyo kutawapa ahueni ya usafiri.

“Niwapongeze Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kuhakikisha meli hizi zinakarabatiwa na kuanza kutoa huduma baada ya kupata changamoto na kusimama kwa zaidi ya miezi 5, kurejea kwa meli hizi sasa watakuwa na uwezo wa kusafiri kwa wakati na kwa gharama nafuu kwa kutumia meli hii’ amesema Naibu Waziri Mwakibete

Naibu Waziri Mwakibete amewataka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu ili kushughulikia changamoto zote zitakazojitokeza kabl aya makabidhiano kati ya TPA na MSCL.

Aidha, Naibu Waziri Mwakibete amewataka TPA kutafuta masoko ili kupata mzigo mkubwa kwa wafanyabiashara ikiwemo Simenti na Makaa ya Mawe ili meli hizo ziweze kuwa na tija na kuongeza pato la Mamlaka.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Kyela Gervas Ndaki ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha meli hizo zinarejea kutoa kutoka huduma katika mikoa iliyo katika Ukanda wa Ziwa Nyasa na kuahidi kuhamasisha wananchi kutumia meli hizo kufanya safari zao.

Naye Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa Manga Gasaya amesema tangu kuanza kutoa huduma kwa meli hiyo idadi ya abiria imekuwa ikiongezeka siku hadi siku na kumuhakikisha Naibu Waziri Mwakibete kuwa TPA ndani ya wiki mbili itatuma wawakilishi kwenda kuzungumza na wafanyabiashara wa nchini Malawi.

Meneja Gasaya ameongeza kuwa TPA kwa sasa meli hizo zinaendeshwa na Mamlaka hiyo na kumuahidi Naibu Waziri Mwakibete kuwa TPA iko kwenye hatua za mwisho  za kukabidhi meli hizo kwa MSCL kwa ajili ya uendeshaji wake kama Serikali ilivyoelekeza.

Serikali kupitia TPA kwa mkoa wa Mbeya imejengwa meli tatu ikiwemo MV. Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200, MV Ruvuma yenye uwezo wa kubeba tani 1000 na MV Ruvuma yenye uwezo wa kubeba tani 1000 meli ambazo zinasafirisha abiria na mizigo kwa Mikoa inayozunguka Ziwa Nyasa na Nchi Jirani ya Malawi.