Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Makandarasi wanawake kutengewa miradi maalum


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameahidi kutenga miradi maalum ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali itakayotekelezwa na makandarasi wanawake.

Waziri Mbarawa amesema hatua hiyo itasaidia makandarasi wanawake kupata uzoefu na kuwajengea uwezo wa kufanya kazi katika miradi mikubwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Prof. Mbarawa amezungumza hayo jijini Dar es Salaam wakati akizundua Chama cha Makandarasi Wanawake (TWCA), kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

“Serikali ina imani na chama hichi  kwani kitaweza kuzalisha watalaamu mahiri na wenye uzoefu wa kufanya kazi kwa pamoja na kuleta tija kwa maendeleo ya sekta ya ujenzi na Taifa kwa ujumla”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa ametoa msisitizo kwa Wizara na Taasisi za Serikali kuzingatia ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na kanuni zake inayotoa kipaumbele kwa makundi maalum hasa kundi la makandarasi wanawake kwa kupata kazi ndogo na kubwa za miradi ya miundombinu inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.

Waziri Prof. Mbarawa, amewataka makandarasi wanawake kutoa fursa za ajira kwa wanawake wenzao kwa ajili ya kuwezeshana na kuongeza nguvu ili kupata kazi zenye viwango na zitakazojitangaza zenyewe.

"Hakikisheni mnawapa kazi makandarasi wadogo ili kuweza kuinuana wenyewe kwa wenyewe na kuzalisha waatalamu mahiri na wenye uwezo wa ushindani", amesisitiza Prof. Mbarawa.

Awali akitoa taarifa ya chama hicho, Rais wa TWCA, Bi. Judith Odunga, amemueleza mgeni rasmi kuwa lengo la kuanzishwa kwa chama hiko ni kuwaunganisha makandarasi wanawake wa kada zote nchini na waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa vifungu vya sera zinazotoa fursa kwa makandarasi wanawake.

Ameongeza kuwa chama hicho kina lengo la kubadilishana uzoefu, changamoto na namna ya kuzizatua kwa pamoja pale zitakapojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao pia kutafuta fursa mbalimbali za mafunzo ya kuwajengea uwezo makandarasi hao.

Hata hivyo, Rais wa TWCA amemuomba Waziri Prof. Mbarawa kuwapatia miradi maalum makandarasi wanawake hao ikiwemo ujenzi wa madaraja na barabara kwa kiwango cha lami ili kufanya kampuni zao ziweze kuwa imara na kuweza kushindana  na kampuni za kinamama za Afrika endapo zitatokea zabuni miradi ya wanawake.

Naye Mlezi wa chama hicho, Rais Mstaafu wa Kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika, Mheshimiwa Mama Getrude Mongela, ametoa rai kwa makandarasi wanawake wote kushika miradi mikubwa kwani wao ni jeshi kubwa na anatarajia kuona mabilionea wakizalishwa kutokea seka hiyo.

Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania (TWCA), kina jumla ya wanachama hai 150 na kimesajiliwa chini ya sheria ya Msajili wa Vyama (Act Cap.337), ya mwaka 2002 na pia kusajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (CRB).