Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Mabaharia wapewe heshima inayostahili- Profesa Mbarawa


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amezungumzia umuhimu wa tasnia ya mabaharia nchini kuthaminiwa na kupewa kipaumbele ili kuwezesha juhudi za Serikali kuhusu uchumi wa bluu kufanikiwa kwa wakati.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya bahari duniani ambayo kitaifa yamefanyika Chakechake Pemba Prof, Mbarawa amesema mafanikio yote ya uchumi wa bluu yatatokana na thamani itakayowekwa kwa mabaharia na wadau wengine wa bahari.

“Asilimia tisini ya biashara za kimataifa hutumia bahari, hivyo ni wajibu wa kila taasisi inayohusika na masuala ya mabaharia kuwathamini na kutatua changamoto zinazowakabili ili kufikia malengo ya nchi na dunia kwa ujumla”, amesema Prof. Mbarawa.

Amewataka mabaharia nchini kuendelea kufanyakazi kwa bidii, nidhamu na   uadilifu ili kuliletea taifa heshima na kutoa fursa nyingi za ajira kwa mabaharia wa Tanzania.

Waziri Prof. Mbarawa amesema Serikali itaendelea kujenga bandari za kisasa katika mwambao wa bahari ya hindi na maziwa makuu na kuongeza idadi ya meli za kisasa katika mkakati wa kuimarisha huduma za usafiri na uchukuzi majini.

Ametoa wito kwa mabaharia wanawake wanaohitimu Chuo cha Mabaharia cha Dar es Salaam (DMI), kupewa kipaumbele katika kazi ili kuondoa dhana kuwa kazi ya ubaharia ni ya wanaume pekee.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), Capt. Musa Mandia ameishukuru Serikali kwa kuamua kuwekeza katika uchumi wa bluu na kusisitiza kuwa mabaharia wakipewa heshima na mahitaji yao yakipatiawa ufumbuzi kwa wakati ni wazi uchumi wa bluu utafanikiwa na kutoa fursa nyingi za maendeleo endelevu nchini.

Siku ya bahari duniani huadhimishwa Alhamis ya mwisho wa mwezi Septemba kila mwaka na ilianza kuadhimishwa miaka 43, iliyopita lengo likuwa kutoa elimu kuhusu umuhimu na usalama wa vyombo vinavyosafiri baharini ambapo mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “mabaharia ni kiini cha maendeleo ya usafirishaji wa baharini siku zijazo”.