Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Kiwanja cha Ndege cha Musoma kukamilika mwakani - Kasekenya


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Musoma utakamilika mwakani hivyo wakazi wa mkoa wa Mara wajipange vizuri kunufaika na fursa zote za ujenzi na matumizi ya kiwanja hicho.

Akikagua upanuzi na ujenzi wa kiwanja hicho kwa kiwango cha lami Eng. Kasekenya amesema lengo la Serikali kurefusha kiwanja hicho na kukijenga kwa viwango vya kisasa ni kuwezesha ndege kubwa  kutua na hivyo kuufungua mkoa wa Mara kwa kuongeza tija katika utalii wa hifadhi ya taifa ya Serengeti.

“Kiwanja hiki kitakapokamilika kitakuwa na urefu wa mita 1,705 na upana wa mita 30 na hivyo kuwezesha ndege nyingi kukitumia na hivyo kuvutia watalii wanaokwenda Serengeti”, amesema Eng. Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amemtaka mkandarasi anayejenga kiwanja hicho Beijing Construction Engineering Group (BCEG), kuzingatia ubora na kukamilisha kazi kwa wakati.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mara Eng. Vedastus Maribe amesema zaidi ya shilingi bilioni 3, za fidia zimeshalipwa na hivyo watahakikisha ujenzi unakuwa wa viwango na unakamilika kama ilivyopangwa.

“Tumejipanga vizuri kupitia msimamizi wa maradi huu (TECU),kuhakikisha mradi unakamilika mapema na kwa viwango vya kimkataba hivyo tunawaomba wananchi watupe ushirikiano”, amesisitiza Eng. Maribe.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya ametoa siku saba kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoa wa Mara kukutana na Mtendaji mkuu wa Wakala huo ili kupitia upya gharama za ujenzi wa jengo la kupumzikia abiria katika eneo la Mwigobero-Musoma ambazo ameelezea kutokuridhishwa nazo.

Amesema hakubaliani na kiasi cha shilingi milioni 86, zilizopangwa kutumika kwani ni kubwa kuliko matarajio ya jengo na eneo husika.

Aidha, amemwagiza Meneja wa TEMESA mkoa wa Mara Eng. Vitalis Bilaul kuhakikisha changamoto za kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma kati ya Mwigobero na Kinesi zinapatiwa ufumbuzi haraka ili kupunguza adha za usafiri kwa wananchi hususan kipindi cha mvua.

Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya siku mbili kukagua miradi ya ujenzi katika mkoa wa Mara.