Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WATUMISHI WIZARA YA UJENZI WAKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA DARAJA LA JANGWANI


Watumishi kutoka Idara na Vitengo mbalimbali vya Wizara ya Ujenzi, wametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Daraja la Jangwani jijini Dar es Salaam, ambao umefikia asilimia 46 ya utekelezaji.

Wakiwa katika eneo la mradi huo, watumishi hao walipata maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Daraja la Jangwani, Kelvin Mobulanga, kuhusu hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.

Mobulanga amesema kuwa nguzo za daraja hilo zimekamilika, huku mkandarasi akiendelea na kazi ya ujenzi wa vitako vya daraja (pile caps).

Ameeleza kuwa daraja hilo lina urefu wa mita 390 na upana wa zaidi ya mita 40, huku kazi zikiendelea katika maeneo mbalimbali ya mradi.

Aidha, amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Mei 2025 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2027. Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kupunguza athari za mafuriko yaliyokuwa yakikumba eneo la Jangwani na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa Barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, watumishi hao pia walitembelea Daraja la Mkwajuni, ambalo ni miongoni mwa madaraja yaliyojengwa kupitia fedha za miradi ya dharura (CERC). Daraja hilo limekamilika kwa asilimia 100.

Ziara hiyo imelenga kuwapa watumishi hao fursa ya kujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara na madaraja nchini.