Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KADOGOSA AMWONDOA MENEJA WA TANROADS SONGWE KATIKA NAFASI YAKE.


 

📌 Ni kufuatia kusuasua kwa Mradi wa upanuzi wa Barabara ya forodha (OSBP) Tunduma

📌Atoa wiki mbili mkandarasi kukamilisha kazi zilizobakia

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amemuondoa katika nafasi yake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Songwe Mhandisi Fredrick Mande, na kumtaka kurejea makao makuu ya TANROADS, kufuatia kushindwa kusimamia ipasavyo mradi wa ujenzi wa barabara ya Forodha - OSBP - Tunduma yenye urefu wa mita 1,675, mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Amesema hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa ili kumpata meneja mwingine atakayesimamia shughuli za TANROADS katika Mkoa wa Songwe.

Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri Kadogosa kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo usiku wa Oktoba 15, 2026, akitekeleza maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ambaye awali alieleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo licha ya Serikali kutoa sehemu kubwa ya fedha za mradi.

Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuboresha mtiririko wa magari na mizigo katika mpaka wa Tanzania na Zambia, Kupunguza msongamano wa magari, kuongeza ufanisi wa huduma za forodha na kurahisisha huduma za biashara za kikanda umeoneshwa kusuasua licha ya kutakiwa kukamilika ifikapo Oktoba 31, 2026 kwa mujibu wa kimkataba.

Aidha, Kadogosa amempa mkandarasi wa mradi huo muda wa wiki mbili kukamilisha kazi zilizobaki, huku akiahidi kurejea eneo hilo ndani ya siku saba kukagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa na kujiridhisha kuwa kasi ya ujenzi imeongezeka.

Kadhalika, Waziri huyo ametoa maelekezo kwa Mameneja wote wa TANROADS nchini kuhakikisha kila mradi wa ujenzi unasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa pande tatu zenye majukumu tofauti, ambazo ni msimamizi wa mradi, mkandarasi na msimamizi anayewakilisha Serikali.

Waziri Kadogosa, ameonya dhidi ya hali ya wasimamizi wa miradi kuegemea maslahi ya upande mmoja, akisema mwenendo huo unaweza kudhoofisha usimamizi huru na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Awali Makamu wa Rais Mhe. Deogratius Ndejembi katika ziara yake, alisisitiza kuwa Serikali inatoa fedha kwa ajili ya miradi ya miundombinu kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, hivyo ni wajibu wa watendaji na wakandarasi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kutoa huduma iliyokusudiwa.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa fedha ili wananchi wanufaike, hivyo tunatakiwa kusimamia kazi ili fedha hizo ziongeze thamani na manufaa kwa wananchi,” alisema Ndejembi.

Alieleza kuwa taarifa alizopokea zilionyesha kuwa mkandarasi alikuwa amelipwa Shilingi bilioni 4.4 kati ya Shilingi bilioni 6.8 za mkataba, sawa na zaidi ya asilimia 60 ya thamani ya mkataba. Hata hivyo, maendeleo ya ujenzi hayakuendana na kiwango cha malipo yaliyokuwa yamefanyika.