Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KIWANJA CHA NDEGE CHA LINDI KUANZA KUBORESHWA.


Serikali imetenga fedha za ndani kiasi cha shilingi takribani bilioni 2 na milioni 600 zikiwa ni kwa ajili ya kuanza taratibu za kuwapata wakandarasi wa upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Lindi.

Akizunguza mara baada ya kutembelea Kiwaja hicho mkoani Lindi, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amesema Serikali imedhamiria kwa dhati kuwezesha miundombinu ya viwanja vya ndege, barabara na bandari kama mkakati wa kuiwezesha miradi mikubwa inayotarajiwa kuanza kutekelezwa mkoani humo.

“Serikali hii chini ya Uongozi wa Rais Mama Samia imeshaelekeza maboresho ya miundombinu ya kimkakati katika mkoa huu yafanyike haraka kama ilivyopangwa mkoani na isipate chongamoto yoyote ile”,amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete ameutaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), kuhakikisha michoro ya kiwanja hicho inazingatia uhalisia wa aina ya miradi ya kimkakati ili kutorudia zoezi hilo.

Kwa upande wake Mbunge wa Lindi Mjini, Mhe. Hamida Abdallah, ameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kuanza mchakato wa kuboresha kiwanja hicho na kusema kukamilika kwa kiwanja hicho kutatochea ukuaji wa uchumi wa mkoa na kuibua fursa mbalimbali zilizopo.

Naye, Mhandisi wa Matengenezo ya Viwanja vya Ndege kutoka (TANROADS)  Mkoa wa Lindi, Ezra Magogo, amesema kwa sasa TANROADS iko kwenye hatua za kupitia michoro iliyopendekezwa na amemuhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa watazingatia maboresho kwani michoro iliyowasilishwa kwa sasa imezingatia ndege aina ya zenye uwezo wa kubeba abiria  takribani 70.

Awali akitoa taarifa ya Kiwanja hicho, Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege vya Mikoa Kutoka TAA, Hamisi Amiri, amesema Mamlaka hiyo na TANROADS zinaendelea kushirikiana kwa karibu kuhakikisha maboresho yanayofanyika kuanzia ngazi ya michoro mpaka kufikia utekelezaji inafanyika kwa kuzingatia miongozo inyotolewa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) ili kuhakikisha viwango vinazingatiwa.

Kiwanja cha ndege cha Lindi kwa sasa kinapokea ndege zisizo za ratiba na kwa mwaka 2021/22 kimeweza kuhudumia abiria zaidi ya 1,000 na ndege zaidi ya 100.