Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KATIBU MKUU UCHUKUZI AWATAKA ATCL KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO


Katibu Mkuu wa Uchukuzi Gabriel Migire amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kuhakikisha anafanya tafiti za mara kwa mara ili kupata suluhu ya changamoto mbalimbali zinazolikabili shirika hilo.

Akizugumza mjini Morogoro wakati wa kufunga Baraza la Wafanyakazi wa ATCL, Katibu Mkuu huyo amesema changamoto hizo zinazohusisha uchelewaji wa ratiba za kuruka na kutua ndege, huduma kwa wateja na  uadilifu zinahitaji ufumbuzi wa haraka kwani zimekuwa zikififisha ubora wa utendaji wa shirika hilo.

“Serikali ilifanya maamuzi ya kulifufua shirika hili kutoka kutokuwa na ndege mpaka kuendesha ndege zaidi ya 10 hivi sasa, lakini kila wakati tumekuwa tukisikia changamoto nyingi kutoka kwa wateja wa ndani na nje ya nchi hivyo katika Baraza hili mpange mikakati ya kuhakikisha changamoto hizi zinapata ufumbuzi mapema", amesisitiza Katibu Mkuu Migire.

Katibu Mkuu Migire amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea mikakati yake ya kulifufua shirika hilo kwa kuhakikisha ndege tano zilizobaki zinakuja ili kulifanya shirika hilo kuchangia katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo na Utalii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi, amesema kwa sasa Shirika limeendelea kukua kwani mpaka sasa kwa mtandao wa ndani shirika linatoa huduma kwa zaidi ya viwanja 12, kanda vituo zaidi ya 6 na nje vituo viwili.

Mhandisi Matindi ameongeza kuwa kwa sasa shirika limekuja na mpango wa miaka mitano ulioanza Julai 2022 hadi June 2026 ambapo msisitizo umewekwa kwenye mpango wa mwaka mmoja wa 2022/23 ambao unajielekeza kuongeza vituo vya ndani kufikia zaidi  ya 19 kutoka vituo 14 vya sasa.

Naye Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa ATCL Bw. Margret Leslie, amesema kwa upande wa wafanyakazi wanaendelea kuchapa kazi kwa weledi na ubunifu ili kuhakikisha Shirika linakidhi vigezo vya utoaji huduma vilivyowekwa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO).

Baraza la wafanyakazi la ATCL limekutana kwa siku mbili  mjini Morogoro ambapo pamoja na mambo mengine  limeweka mipango mbalimbali ya kuimarisha utoaji wa huduma nchini na nje ya nchi.