Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KASEKENYA: TUMIENI WATAALAM ACHENI KUOGOPA GHARAMA


Serikali imetoa wito kwa Mashirika, Taasisi za Serikali pamoja na Sekta Binafsi kushirikisha watalaam wa fani ya Wabunifu Majengo katika utelelezaji wa miradi mbalimbali ya majengo, barabara na madaraja ili kuleta ubunifu wa kipekee katika miji na kuifanya iwe yenye mandhari bora.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, katika Mkutano wa 27 na Kumbukizi ya Miaka 40 ya Chama cha Wabunifu Majengo Tanzania (AAT), ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza elimu zaidi itolewe kuhusu umuhimu wa tasnia hiyo katika shughuli za ubunifu wa majengo hasa kwa Sekta Binafsi.

“Niseme tu kama mtanzania wakati fulani hatutumii sana wataalam ambao mwisho wa siku utapata kazi yako nzuri, ya uhakika na yenye usalama kwa kuhofia gharama kubwa na matokeo yake tunaenda kwa watu wa barabarani bila kufahamu athari zake hivyo ni jukumu lenu kuwaelesha wananchi kuhusu fani hii”, amesema Eng. Kasekenya.

Kasekenya ameonesha umuhimu wa Wataalam hao kuungana pamoja ili kushiriki katika miradi mikubwa na kujijengea uwezo ili kuipunguzia nchi utegemezi wa wataalam kutoka nje wakati wa ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara, madaraja na majengo ambayo inajengwa kwa gharama kubwa.

Amewataka Wabunifu Majengo waliosajiliwa na chama hicho kuwa wataalam wabobezi watakaotoa huduma nzuri iliyo bora na kwa gharama nafuu kwa wananchi, Sekta Binafsi na Serikali.  

“Hatutegemei Mbunifu majengo aliyesajiliwa na AAT chini ya usimamizi wenu kutoa huduma chini ya kiwango na isiyokuwa na maadili mazuri”, amesisitiza Eng. Kasekenya.

Aidha, Kasekenya amesema Wizara imechukua ombi la ushirikishwaji wa Wabunifu Majengo katika usanifu wa barabara, madaraja, vituo vidogo vya mabasi, miundombinu ya njia za waenda kwa miguu ili kupata mandhari nzuri ya miji  kwa upande wa miundombinu kama nchi za wenzetu.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Arch. Edwin Nnunduma amewataka Wabunifu Majengo nchini kutafakari katika kipindi cha miaka 40 ya Chama hicho kama malengo yao yametimia ikiwemo ya utoaji wa huduma bora ya majengo.

Arch. Nnunduma amekitaka Chama hicho kuja na mikakati ya kuijenga tasnia hiyo ya Wabunifu Majengo ikawe ya Ushindani ndani na nje ya nchi.

“Bodi inategemea Chama hiki kiende mbele zaidi ya majukumu ya Bodi na hasa katika kutoa huduma bora kwa umma, kubaini mapungufu yaliyopo kwa wataalam na tasnia yenyewe na kuwasilisha Serikalini kwa lengo la kuongeza idadi ya wataalam weledi na wenye uzoefu na kuweza kuaminiwa zaidi katika uvumbuzi, usimamizi na kutoa mafunzo”, amefafanua Arch. Nnunduma. 

Naye, Rais wa Chama cha AAT, Arch. David Kibebe, ameishukuru Wizara ya Ujenzi kwa kushughulikia suala la kuandaa sheria za ujenzi ambazo Chama imekuwa ikilizungumzia kwa kipindi kirefu.

Arch. Kibebe ameeleza kuwa Chama kwa kushirikiana na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi wamekuwa kiungo kikubwa katika kutoa mafunzo kwa vijana wanaotarajia kusajiliwa na bodi hiyo kwa mujibu wa Sheria.

Chama cha Wabunifu Majengo Tanzania (AAT), kiliundwa rasmi Mwaka 1982 ambapo kilikuwa na wanachama wasiozidi 15 ambapo mpaka kimesajili jumla ya wanachama 1,200 kikiwa na lengo la kuhakikisha fani hiyo inaendelezwa na inafanywa kwa weledi ili kutoa huduma bora kwa jamii na Serikali.