Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KASEKENYA: MADEREVA WA SERIKALI WATAKIWA KUENDANA NA TEKNOLOJIA MPYA ZA MAGARI


Serikali imehimiza mafunzo endelevu kwa madereva wa Serikali ili kuwawezesha kuendana na matumizi ya magari ya kisasa yenye teknolojia mpya, ambayo yameleta mabadiliko makubwa katika mifumo ya uendeshaji na matengenezo ya magari nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, leo Septemba 16, 2026, wakati akifungua Kongamano la Tano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST).

Mhandisi Kasekenya amezitaka Taasisi za Umma kutenga bajeti kwa ajili ya mafunzo ya mara kwa mara kwa madereva, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa madereva kuhusu matumizi sahihi ya magari mapya, kupunguza uharibifu unaoweza kuepukika, kuongeza usalama barabarani na kulinda thamani ya mali za Serikali.

“Niwahakikishie kuwa Serikali inatambua maendeleo ya teknolojia katika Sekta ya Usafiri na umuhimu wa mafunzo yake kwa madereva wa Serikali. Niwaombe muendelee kuwa na utayari wa kujifunza, kuzingatia maadili ya kazi na kutumia kwa uangalifu magari hayo ili kuongeza ufanisi,” amesema Mhandisi Kasekenya.

Aidha, Mhandisi Kasekenya amewataka madereva wa Serikali kuendelea kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani, pamoja na kuanza mchakato wa kuhuisha leseni zao mapema kabla ya muda wa uhalali kuisha.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Qs. Mwanahamis Kitogo, amewataka madereva wa Serikali kuzingatia maadili, kuongeza umakini na kuzingatia weledi katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa usalama wa viongozi na watumishi wa umma unategemea kwa kiasi kikubwa utendaji wao.

Kitogo amewataka madereva kutambua kuwa magari wanayokabidhiwa ni nyenzo muhimu za kazi zinazopaswa kutunzwa na kutumiwa kwa uangalifu, ili kupunguza gharama za Serikali zinazoweza kujitokeza kutokana na ununuzi wa magari mapya unaosababishwa na uharibifu au matumizi yasiyo sahihi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania, Said Kapande, ameishukuru Serikali kwa kutoa ajira mpya 1,022 kwa madereva katika Ikama ya mwaka wa fedha 2025/26, akisema hatua hiyo itaimarisha utoaji wa huduma kwa maofisa wa Serikali na wananchi.

Kapande amesema Tanzania ina jumla ya madereva wa Serikali 10,072, wakiwemo wanawake 63 na wanaume 10,009. Aidha, amebainisha kuwa tangu kuanza kutumika kwa muundo mpya mwaka 2023, madereva 3,175 walipandishwa vyeo, huku ajira 1,430 zikitolewa katika mwaka wa fedha 2024/25.