Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KASEKENYA AWATAKA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO KWA MKANDARASI KUHARAKISHA UJENZI WA NJIA NNE MBEYA


Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amezungumzia umuhimu wa wananchi na wadau wengine wa miundombinu kutoa ushirikiano kwa wakandarasi pale wanapohamisha ili kuwezesha ujenzi wa barabara kufanyika kwa haraka.

Akizungumza jijini Mbeya wakati akikagua ujenzi wa barabara ya njia nne (Nsalaga -Ifisi Km 29), Eng. Kasekenya amesema kasi ya ujenzi wa barabara hiyo itaongezeka baada ya kazi kubwa ya kuhamisha miundombinu ya maji, umeme na mkongo wa mawasiliano kukamilika kwa kiwango kikubwa.

“Tumejipanga kuhakikisha ujenzi wa barabara hii unakwenda kwa haraka kabla ya mvua kubwa kuanza ili kuwezesha wananchi na wasafirishaji kunufaika na barabara hii ambayo ni muhimu kwa uchumi wa mikoa ya Mbeya, Songwe na taifa kwa ujumla” amesema Eng. Kasekenya.

Amemhakikishia Mkandarasi CHICO anayejenga barabara hiyo kuwa Serikali inaipa kipaumbele barabara hiyo na malipo ya kazi zilizokamilika yatafanyika haraka kadri ili kutochelelesha ujenzi huo.

Amemtaka Mhandisi Mshauri TECU kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa ubora uliokusudiwa wakati wa usanifu ikizingatia ni barabara ya kiuchumi na inayopitisha magari mengi wakati wote wa mwaka.

Zaidi ya shilingi bilioni 138 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara ya Igawa-Songwe-Tunduma yenye urefu wa KM 218 inayounganisha Tanzania na Zambia na kukamilika kwake kutachochea fursa za uchumi katika mikoa ya Mbeya na Songwe na kurahisisha usafiri jijini Mbeya.