Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KASEKENYA AWAAGIZA TANROADS KUFUNGUA MAWASILIANO YA DARAJA LA MTO RUKWA


Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameutaka Wakala wa Barabara Nchini ( TANROADS), kuhakikisha wanafungua mawasiliano ya Barabara la kutoka Katavi kwenda Songwe kupitia Bonde la Mto Rukwa.

Kasekenya ameyasema  hayo leo wakati akikagua daraja hilo ambalo limeathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha na hivyo kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya mikoa hiyo.

“Niwaagize TANROADS kuhakikisha kazi inaendelea bila kusimama na mawasiliano yanarudi kama ilivyokuwa hapo awali, maana daraja hili ni muhimu kwa wananchi wa kata ya Mto wisa na kata ya Zimba,lakini pia na mkoa wa Rukwa na Songwe kwa ujumla” amesema Kasekenya.

Aidha, Kasekenya ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya barabara ili iweze kuendelea kutumika na kuacha kufanya kazi kwenye vyanzo vya maji, kwani barabara ni za wananchi wenyewe na sio za Serikali.

Katika Upande mwingine, amewataka TANROADS na Bodi ya Mfuko wa Barabara,( ROAD FUND) kuhakikisha wanazitembelea barabara mara kwa mara katika kipindi hiki cha mvua za El nino.

“ TANROADS na ROADS FUND kuna haja kubwa  kupita kwenye haya maeneo ya barabara na madaraja kupata tathmini ya mahitaji na changamoto ili wanapokuja kuomba fedha za dharura waweze kupewa ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwa haraka”, amesema Mhandisi Kasekenya.

Kwa upande wake, Meneja wa  TANROADS Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Mgeni Mwanga amesema tayari timu ya wataalamu kutoka sehemu mbalimbali wameshafika na wanahakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kurudisha mawasiliano ya daraja hilo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Bw. Nyakia Ally amesema kuwa mvua kubwa iliyonyesha imesababisha  madhara kwenye mashamba, nyumba, barabara pamoja na madaraja na wanawashukuru TANROADS kwa kuweza kuanza kazi ya kurejesha daraja lililokatika.

“ Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita, kupitia Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kuweza kutujengea daraja la muda tukiwa tunasubiria kurejeshewa kwa daraja la  awali ambalo mawasiliano yake yamekatika” amesema Nyakia

Kurejeshwa kwa daraja la mto Rukwa ambalo linakunganisha Mkoa wa Rukwa, Katavi na Songwe kutaimarisha uchumi, biashara na uwekezaji wa wananchi katika  mikoa hiyo