Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Kasekenya amtaka mkandarasi Daraja la JPM kufidia muda ulipotea


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15 Bureau Group Corporation wanaojenga Daraja la JPM (Kigongo hadi Busisi), lenye urefu wa kilometa 3.2 kufidia muda uliopotea na kuwafanya wawe nyuma kwa asilimia 7.

Akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa daraja hilo linalounganisha wilaya za Misungwi na Sengerema jijini Mwanza, Naibu Waziri Kasekenya amebaini kuwepo kwa ucheleweshwaji wa mradi huo kutokana na changamoto mbalimbali ambapo kwa sasa mradi umefikia asilimia 29 huku mpango kazi wa ujenzi wake ukiitaka kazi hiyo kuwa imefikia asilimia 36.

“Hakikisheni mnafidia muda uliopotea kwa kuongeza nguvu kazi au vitendea kazi na ikiwezekana mfanye kazi ya ujenzi wa daraja hili usiku na mchana ili kuhakikisha daraja hili si tu linakamilika ndani ya miezi 48, lakini pia linakamilika kwa viwango vilivyo ainishwa kwenye mkataba ili liweze kudumu kwa miaka 120 kama ilivyokusudiwa”, amesema Mhandisi Kasekenya.

Ameongeza kuwa ujenzi wa Daraja la JPM (Kigongo - Busisi), ukikamilika unatarajiwa kuibua fursa za biashara na kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza, mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa lakini pia nchi jirani za Rwanda, Uganda na Burundi.

Naibu Waziri huyo amewataka watanzania kutembea kifua mbele na kujivunia mradi huo mkubwa unaotelekezwa kwa fedha za Serikali ya Tanzania, yaani fedha halali ya walipakodi, ambapo kwa sasa tayari umetoa ajira kwa idadi kubwa ya watanzania na kuwapa fursa za kibiashara wananchi wa maeneo ya jirani na mradi huo.

Aidha, Mhandisi Kasekenya amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa malipo ya mradi huo kila inapofikia hatua ya malipo na kwamba kwa hatua iliyofikiwa Serikali haidawi.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya Afrisa Consulting Ltd, Mhandisi Benjamin Michael, amemueleza Naibu Waziri Kasekenya kuwa ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi uko nyuma kwa asilimia 7 kutokana na changamoto ya kuwepo kwa mwamba chini ya maji ambapo awali haukuonekana, lakini pia changamoto ya maji kujaa ziwani kwa urefu wa zaidi ya mita 2 kwenye ziwa hali iliyolazimu kuongezeka urefu wa nguzo za daraja hilo na kwamba kwa sasa ujenzi unaendelea usiku na mchana ili kufidia muda uliopotea.

Naye, Msimamizi wa mradi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), jijini Mwanza, Mhandisi William Senga, amefafanua kuwa gharama za mradi wa ujenzi wa daraja hilo ni Shillingi Bilioni 716.3 ambapo gharama za Mkandarasi ni Shilingi Bilioni 699.2, Mhandisi Mshauri ni Shilingi Bilioni 11, Usanifu ni Shilingi Bilioni 2.8 na fidia kwa wananchi waliopisha maeneo ya barabara za maingilio kwenda kwenye daraja hilo ni Shilingi Bilioni 3.1.

Jiji la Mwanza linatarajiwa kuwa kitovu cha biashara na utalii kutokana na kuwepo kwa miradi mingi mikubwa inayoendelea ikiwemo mradi wa ujenzi wa Daraja la JPM (Kigongo - Busisi), ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR (Mwanza hadi Isaka) na ujenzi wa Meli kubwa ya kisasa ya MV. MWANZA ‘Hapa Kazi Tu’.