Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KASEKENYA AAGIZA TANROADS KUTENGENEZA MAENEO KOROFI


Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amewaagiza Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), nchini kutoa kipaumbele katika kutengeneza maeneo korofi ya barabara na madaraja ili yaweze kupitika kipindi chote cha mwaka.

Ameyasema hayo jijini Dodoma katika kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Wakala huo ambapo amewakumbusha wajibu wao katika utekelezaji wa majukumu yao ili kutoa mchango mkubwa kwa Taifa.

“Miundimbinu ya barabara ni kichocheo katika ukuzaji wa Sekta nyingine hivyo hakikisheni mnajenga na kukarabati maeneo yote korofi ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji”, amesisitiza Eng. Kasekenya.

Aidha, Eng. Kasekenye ameagiza uongozi wa TANROADS kutoa elimu kwa wasafirishaji na wadau wote wanaotumia miundombinu ya barabara nchini kutomwaga mafuta, michanga, mawe na kokoto ambavyo vinapelekea kuharibu miundombinu hiyo.

Amewataka Mameneja hao kuendelea kuwa wabunifu, waadilifu na kusimamia kazi zao kwa ubora na kwa wakati ili kuleta matokeo chanya yatakayopelekea Sekta ya Ujenzi kupiga hatua kubwa.

“Endeleeni kutumia utaalamu wenu katika ujenzi na usimamizi wa miradi ili kuwa na miundombinu bora itayokidhi mahitaji ya vizazi vya sasa na vijavyo”, amefafanua Eng. Kasekenya.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Eng. Kasekenya, Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Ujenzi, Balozi Mha. Aisha Amour ameeleza kuwa lengo la kikao hicho ni kujadili na kushauri namna bora ya kutatua kero za watumiaji wa miundombinu ya barabara ikiwemo kupeana mbinu mbalimbali za kutatua kero hizo.

Amezitaja baadhi ya kero hizo kuwa na uwepo wa matuta yasiyo na viwango, mashimo kwenye barabara na uwekaji wa alama usio sahihi katika mahali husika.

“Kikao hichi kinalenga zaidi katika kazi za matengenezo ya barabara, miradi ya maendeleo inayoendelea, usalama barabarani na matukio ya ajali hivyo tumieni fursa hii kuleta mwazo chanya yatakayoikuza Sekta”, amefafanua Balozi Aisha.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Dar es Salaam, Eng. Haroun Senkuku, ameeleza kuwa ofisi yake inatarajia kuongeza barabara za juu (flyover) nyingine tatu (3) ili kupunguza msongamano wa magari yanayoingia na kutoka katika jiji hilo.

Naye, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Kilimanjaro, Eng. Motta Kyando, ameeleza kuwa kazi za matengenezo ya barabara katika mkoa huo kwa mwaka wa fedha 2021/22 zimekamilika kwa asilimia 95 na kwa sasa hali ya barabara katika mkoa huo ni nzuri kwani inapitika majira yote ya mwaka.

Meneja wa TANROADS, mkoa Katavi, Eng. Martin Mwakabende, ameeleza kuwa mkoa huo unahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 1,195 ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 wamepanga kutekeleza miradi 39 kati ya hiyo miradi 31 tayari imepata wakandarasi.