Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Kamilisheni kazi kwa wakati: Prof. Mbarawa


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amemwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Arusha Eng. Reginald Masawe kuhakikisha ujenzi wa mizani ya kisasa ya Kimokouwa iliyoko wilayani Longido unakamilika haraka.

Mizani hiyo ya kisasa itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kupima magari yakiwa katika mwendo (weigh in motion), na hivyo kuondoa msongamano wa magari katika mpaka wa Namanga unaounganisha Tanzania na Kenya.

“Wiki sita zitawatosha kukamilisha kila kitu na kazi ianze ili kuondoa msongamano na kero kwa wasafirishaji”, amesema Prof. Mbarawa.

Mradi huo unaojengwa na kampuni ya CRJE ya China na kusimamiwa na Ambicon ya Dar es Salaam utakapokamilika utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 14.7   na unatarajiwa kutoa fursa nyingi za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa wilaya ya Longido.

Amewataka wote watakaopewa nafasi katika mradi huo kufanya kazi kwa bidii, nidhamu, uzalendo na kuepuka vitendo vya rushwa.

Naye Mbunge wa Longido Dkt. Stephen Kiruswa amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuchangamkia fursa za ajira na biashara ili kukuza uchumi wao.

Amewataka wakazi hao kulinda na kuitunza miundombinu inayojengwa na Serikali kwani hutumia gharama kubwa.

Ujenzi wa mizani ya Kimokouwa  ya kupima magari yakiwa katika mwendo (weigh in motion), ni mkakati wa Serikali kupunguza msongamano katika maeneo yote ya mizani hususan mipakani ili kuharakisha huduma za usafiri na uchukuzi nchini.